MAJAMBAZI WALIOBAKA WAKE ZA WATU KWA ZAMU (Mande),KUPORA NA KUJERUHI WAFUNGWA MIAKA 242 JELA -SHINYANGA

 

Mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga imewahukumu Mathias Kalonga(40) na James Moshi(35) wakazi wa kijiji cha Shatimba wilaya ya Shinyanga vijijini kutumikia kifungo cha miaka 242 jela baada ya kupatikana na kosa la ubakaji kwa mande(kubaka kwa mpigo),wizi wa kutumia silaha  pamoja na kujeruhi.


Mwendesha mashtaka,wakili wa serikali Salome Mbuguni aliiambia mahakama hiyo jana kuwa mnamo tarehe 18 mwezi Oktoba mwaka 2012 washtakiwa Mathias Kalonga na James Moshi wakiwa na wenzao walivamia nyumbani kwa mlalamikaji Lesha Jidomela,wakiwa na bunduki na mapanga kisha kumjeruhi kwa kumpiga ubapa wa panga usoni na shavuni kisha kupora simu 3 kinyume cha sheria hilo ikiwa ni kosa la kwanza na la pili.

Wakili huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa katika kosa la tatu na nne washtakiwa hao wote kwa pamoja  walivamia nyumbani kwa Sayi Jidomela(ndugu yake na Lesha Jidomela) kisha kupora shilingi 57,000/=  na simu moja na mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa na panga kumjeruhi Sayi Jidomela kwa kutumia panga hilo.

Mwendesha mashtaka Mbuguni alisema katika kosa la tano na sita washtakiwa kwa pamoja walimbaka mke wa Lesha Jidomela kwa pamoja(mande),lakini pia wakambaka mke wa Sayi Jidomela kwa pamoja (mande) kinyume cha sheria.

Akitoa hukumu,hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Shinyanga Thomson Mtani alisema kutokana na kosa la wizi wa kutumia silaha kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela, hivyo kila mmoja jumla ya miaka 60 kila mmoja kwani walitenda kosa hilo katika nyumba mbili.

Hakimu Mtani alisema katika kosa la ubakaji kwa mande kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela,na kwa kuwa wote kwa pamoja walibaka wanawake wawili kwa zamu kila mmoja jumla ya miaka atakayotumikia  jela ni miaka 60.

Hakimu huyo aliongeza kuwa mshtakiwa wa kwanza Mathias Kalonga atatumikia kifungo cha miaka 2 mingine jela kwa kosa la kujeruhi kwa panga na kutakiwa kulipa fidia ya shilingi laki mbili kwa waliojeruhiwa.

Kufuatia hukumu hiyo washtakiwa watatumikia kifungo cha miaka 242 jela,ambapo mshtakiwa wa kwanza Mathias Kalonga(40) atatumikia miaka 122 jela na mshtakiwa wa pili James Moshi(35) atatumikia miaka 120 jela na wote kwa pamoja kuchapwa viboko 12 kila mmoja.

Hata hivyo mahakama ya hakimu mkazi Shinyanga imewapa nafasi washtakiwa hao kukata rufaa kwa hukumu hiyo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post