LISU NA ROSE MUHANDO WAWASHUKURU WATANZANIA WAPIGA KURA

Rose Muhando
John Lisu

WAKATI zoezi la upigaji kura wa kuchagua maeneo matatu ya kufanikisha Tamasha la Pasaka linalotarajia kufanyika kuanzia Aprili 20 mwaka huu, waimbaji mahiri wa muziki wa injili hapa Tanzania, Rose Mhando na John Lisu wameonesha shukrani kwa wapiga kura kwa kuwapigia kura nyingi kuelekea tamasha hilo.

Waimbaji hao wanaoonesha kukubalika na wadau mbalimbali kushiriki katika tamasha hilo kutokana na sababu mbalimbali za uwasilishaji wao wa Neno la Mungu kwa wadau wa tamasha hilo, ingawa zoezi hilo likiendelea. John Lisu amewashukuru Watanzania kwa kuonesha kumkubali katika utoaji wake wa huduma za kufanikisha Neno la Mungu kupitia uimbaji wa nyimbo za injili, huku zoezi la upigaji kura likiendelea.

Lisu anasema Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama amekuwa baraka kwa Mungu kwa sababu amekuwa akitumia gharama kubwa kuwaleta waimbaji mbalimbali wa Kimataifa katika tamasha hilo. “Mchango wa Msama kwa jamii ni mkubwa hasa katika maendeleo, hivyo natoa shukrani kwa Msama kwa kufanikisha kufanyika kwa matamasha ya kufikisha neno la Mungu ambayo ni Pasaka na Krismasi,” alisema Lisu.

Rose Muhando amesema kupata kura nyingi ambazo zinaashiria kipimo cha kuonekana na Mungu  na watu mbalimbali wanaopenda kazi za mikono yake kwamba anastahili kutoa huduma ya Neno la Mungu katika tamasha hilo.

Muhando anasema kwa sababu Mungu na Watanzania wameona umuhimu wa yeye kushiriki kutoa huduma katika tamasha hilo, anawashukuru kwa hatua hiyo ingawa zoezi bado linaendelea, kwani ni mwelekeo mzuri kwao kuelekea katika tamasha hilo. “Namshukuru Mungu na watanzania wenzangu walionipigia kura kwa wingi ikiwa ni njia pekee ya kufanikisha kuhudumu katika Tamasha la Pasaka,” alisema Muhando.

Muhando anasema sababu zinazofanikisha kupata uteuzi wa mara kwa mara ni kwamba mara nyingi anapenda kazi yake ijieleze yenyewe na anaamini kwamba kazi yake inatamka neno ambalo linagusa mioyo ya wanadamu ambao wanatakiwa kumfikishia Mungu matatizo yao. Anatumia fursa hiyo kuishukuru kampuni ya Msama Promotions kwa kufanikisha matamasha ya kumuimbia na kumtukuza Mungu kupitia waimbaji mbalimbali wa kitaifa na Kimataifa ambao kwa pamoja wanatoa elimu kwa jamii kuhusu kumuabudu Mungu.

Muimbaji huyo amesema atajisikia vibaya iwapo atakosa nafasi ya kufikisha ujumbe wa neno la Mungu kwa sababu tamasha hilo ni kubwa kwani hata ingekuwa kuhudumu bure yuko tayari kwa sababu ibada yake inafika vilivyo kwa Mungu kwa sababu ya wingi wa wanaohudhuria. Muhando anatumia fursa hiyo kuwaeeleza Watanzania kwamba iwapo atapata nafasi ya kuwemo kwenye orodha ya waimbaji katika tamasha hilo, atawasilisha albamu yake ya tano ya Kamata Pindo la Yesu yenye nyimbo nyingi ikiwemo Facebook.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama waimbaji hao wamepigiwa kura na wadau wa muziki huo ambao wanakubali kazi zao.
Msama amesema  Tamasha la Pasaka la mwaka huu limekuja katika mfumo mwingine kabisa ambao ni wa upigaji kura ili kuchagua maeneo matatu yatakayofanikisha kufanyika kwa tamasha hilo ambalo limekuwa likitumika katika kufanikisha kuwasaidia wenye uhitaji maalum ambao ni pamoja na wajane, walemavu na yatima.

Kupitia matamasha yanayoandaliwa na Msama, viingilio vinavyopatikana katika matamasha hayo vinafanikisha mipangilio ya kujenga kituo cha wenye uhitaji maalum katika eneo la Pugu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambacho kinajulikana kama Jakaya Mrisho Kikwete, rafiki wa wasiojiweza.
Msama anasema kwa kuanzia kuelekea tamasha hilo linalotarajia kuanza Aprili 20 jijini Dar es Salaam, ambalo litaendelea katika mikoa mingine zaidi ya nane hapa nchini ambapo kauli mbiu ya tamasha hilo ni ‘Uzalendo Kwanza, Haki huinua Taifa’ inayochochea na kuimarisha amani na kudumisha maendeleo ya Tanzania ijayo.

Msama anatoa wito kwa kuwakumbusha Watanzania namna ya kuwapigia kura wahusika ambapo utaratibu wa kupiga kura tayari umebainishwa kwa wale ambao watahitaji kufanya hivyo kwa kuandika Pasaka acha nafasi kisha andika jina la mwimbaji unatuma kwenda namba 15327.

Pia kwa mgeni rasmi  andika neno Pasaka acha nafasi kisha andika jina la mgeni rasmi unayetaka kumpigia kura tuma kwenda 15327, wakati mikoa unaandika Pasaka acha nafasi jina la mkoa unaotaka kuupigia kura tuma kwenda namba 15327,  pia imebainishwa kuwa kila mmoja anaruhusiwa kupiga kura kadri awezavyo ili kupata mwimbaji na mgeni rasmi na mkoa husika ili tamasha hilo liweze kufanyika katika mkoa husika.

Msama anasema mojawapo ya  wadhamini wa tamasha hilo ni magazeti ya Dira ya Mtanzania na Pata Habari ambayo ni sehemu ya kampuni ya Msama Promotions na kutoa wito kwa wadhamini wengine kujitokeza kufanikisha tamasha hilo.
“Tamasha la Pasaka linahitaji wadhamini wengine ambao watasaidia kufanyika kwa ufanisi, hivyo wajitokeze kutusaidia kufanikisha, kwa sababu lina nia njema kwa Tanzania,” alisema Msama
credit-dar es salaam

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post