Siri yafichuka!!! WATUMISHI WA MANISPAA YA SHINYANGA WADAIWA KUBUNI NJIA MPYA YA ULAJI,UTITIRI WA KESI WAIGUBIKA MANISPAA HIYO

Baadhi ya watumishi katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga wamedaiwa  kuihujumu kwa kutumia mbinu ya kufungua kesi dhidi ya manispaa hiyo na kuiba nyaraka za ofisi ili kujipatia kipato kinyume cha taratibu na maadili ya kazi.

Akizungumza  katika kikao cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo,kilichofanyika jana katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga, mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia naibu mstahiki meya wa manispaa hiyo David Nkulila(PICHANI HAPO JUU) alisema halmashauri hiyo tofauti na siku za nyuma sasa inaandamwa na kesi nyingi za ajabu ajabu zenye lengo la kuihujumu.

“Manispaa ya Shinyanga hivi sasa  inataka kuchezewa na baadhi ya watu kwa kuanzisha makosa yasiyoeleka dhidi ya manispaa na mujibu wa taarifa zinazohisiwa,zinazotia mashaka hujuma hizo zinafanywa na watumishi wa halmashauri”,alieleza mwenyekiti wa baraza hilo bwana Nkulila.

“Data zinazohisiwa,zinazosemekana,zinazotia mashaka,watumishi wanahusika,Kesi nyingi sasa zinataka kuiandama halmashauri,mdau yupo anaambiwa anzisha kesi na kesi inaenda kushindikana,mtu huyo anadai alipwe na halmashauri, na hayo madai yanavyosemekana ni mgao wa watu,hizo ni hujuma kwa pesa za wananchi”,alisema Nkulila.

Akifafanua zaidi alisema menejimenti ya manispaa hiyo imekosa nidhamu ya siri kwani wamekuwa wakitoa nyaraka za siri na kwamba sasa wamebuni njia nyingine ya ulaji kwa kuanzisha kesi badala ya kuwajibika.

“Katika uongozi wangu haya nimeyaona,hata mkurugenzi wa halmashauri wa manispaa ni shahidi,mtu anacheza na kitu anachojua kabisa kuwa ni makosa,anaiba nyaraka ,akishaiba anaenda wanashauriana na wenzake ,analeta malalamiko,akitaka nini alipwe ”,alieleza Nkulila.

“Zimeanza kuibuka kesi ambazo katika halmashauri haziwahi kutokea,hizi ni hujuma tu,hujuma ya nini?,ulaji!,ulaji kivipi? nyofoa nyaraka hii....,hili lazima tulikemee,lazima tuliseme,tutakwenda nao sambamba,mimi niko pale nimepewa dhamana ninayaona kila siku,hawa hawhitaji kuletwa kwenye baraza ni kuwapeleka mahakamani tu”,aliongeza naibu meya huyo.

Aidha alisema aina hiyo ya wizi inatokana na pale watendaji wanapowajibishwa na inapotokea kibano cha ulaji katika kila eneo kimeshindikana, basi wameamua kubuni njia nyingine ya ulaji kwa kufungua kesi za ajabu ajabu dhidi ya manispaa ili mwisho wa siku walipwe mamilioni ya fedha ambayo kimsingi ni mali ya wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi alieeleza kukerwa na tabia hiyo na kuwataka watumishi wa umma kutunza siri za ofisi na endapo mtu anaona kazi ya serikali ni ngumu basi aache badala ya kuchezea nyaraka za serikali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post