Kwa mara ya kwanza Shinyanga!! MIGODI YA BUZWAGI NA BULYANHULU YAKUTANA NA WAFANYABIASHARA LEO MJINI SHINYANGA

Siku chache tu baada ya bwana Philbert Rweyemamu(Muafrika) kuwa meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi ulioko wilayani Kahama kwa mara kwanza wafanyabiashara mkoani Shinyanga wamekutana katika mkutano wa pamoja na migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu katika ukumbi wa hoteli ya Karena iliyoko mjini Shinyanga kujadili masuala mbalimbali ya kibiashara na namna gani wafanyabiashara hao wanaweza kunufaika na migodi inayowazunguka lakini pia kujadili mpango wa migodi hiyo kuendeleza wagavi wa ndani ya nchi na fursa zinazotolewa na migodi hiyo.

Mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Allya Nassoro Rufunga ambaye ametumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara mkoani Shinyanga kutumia fursa za kibiashara zinazotolewa na migodi ya kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu  African Barrick (ABG) ili kuinua biashara zao na kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

 Katika mkutano wa wafanyabiashara wa mkoa wa Shinyanga na migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu iliyopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Rufunga  amesema ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya wafanyabiashara kuhusu kutopewa fursa ya kufanya biashara na migodi hiyo jambo ambalo limekuwa likikwamisha ukuaji wa biashara zao.

Amesema kupitia fursa zinazotolewa na migodi hiyo ni vyema wafanyabiashara wakazitumia kama inavyotakiwa kwani migodi hiyo ipo katika maeneo yao na haibagui mtu yeyote na kwamba hata wafanyabiashara wa nje ya mkoa wanaruhusiwa kufanya biashara na migodi hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema serikali itaendelea kushirikiana na migodi huku akiwataka wafanyabiashara kufika katika ofisi za mkoa kama wanapata matatizo na kuongeza kuwa sekta ya madini ni miongoni mwa  sekta zitakazosaidia kuinua uchumi wa mkoa wa Shinyanga ukiachilia mbali kilimo na viwanda.

Kwa upande wake meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi Philbert Rweyemamu amesema lengo mkutano huo ni kukutana na wafanyabiashara hao ili kuwaelimisha kuhusu fursa mbalimbali za kibiashara zinazotolewa na migodi hiyo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanafaidika nayo.

Rweyemamu ambaye ni meneja wa kwanza wa kiafrika kuongoza migodi amesema kampuni yake inalenga katika kushirikiana na wafanyabiashara wa ndani kuendeleza uchumi wa nchi na kutoa fursa katika ngazi ya jamii za kujishughulisha katika biashara ili kuongeza kipato katika familia.Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya African Barrick kukutana na wafanyabiashara mkoani Shinyanga na imeahidi kuuendelea kukutana na wafanyabiashara kila mwaka ili kuangalia namna gani wananchi wanaozungukwa na migodi wafaidike na madini yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post