Je? Tutafika!!! KAMATI YA SHULE YATUNISHIANA MISURI NA UONGOZI WA SHULE YA MSINGI BUGOYI B ILIYOPO KATIKA MANISPAA YA SHINYANGA

 Ni katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata ya Ndembezi mjini Shinyanga ambako leo kumefanyika kikao cha dharura kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo ikiwemo suala la mgogoro uliopo kati ya uongozi wa shule ya msingi Bugoyi B iliyopo katika manispaa ya shinyanga na kamati ya shule hiyo.Aliyesimama ni diwani wa kata ya Ndembezi ambaye pia ni naibu meya wa manispaa ya Shinyanga Ndugu David Nkulila akifungua kikao hicho.Aliyekaa ni afisa mtendaji wa kata hiyo ndugu James Dogani


Aliyesimama ni mwenyekiti wa kijiji cha Ndembezi ndugu Jumanne Maziku akichangia mawili matatu katika kikao hicho.Aliyekaa ni Chifu Abadallah Sube ambaye ni mwenyekiti wa mtaa wa Mbuyuni ilipo shule ya msingi  Bugoyi B ambayo imegubikwa na mgogoro kati ya uongozi wa shule hiyo hali inayopelekea kurudisha nyuma maendeleo ya shule hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo na wanafunzi kukaa chini pamoja na kwamba shule hiyo iko mjini

Wajumbe wa kikao hicho cha dharura wakifuatilia kilichokuwa kinajiri ndani ya kikao hicho
Kulia ni mwalimu mkuu wa shule ya Bugoyi B ndugu Anord Rweshabura,kushoto ni mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo ndugu Hosea Mbusule ambaye alikiambia kikao hicho kuwa kamati yake haikuwa ikishirikishwa ipasavyo katika masuala ya maendeleo shuleni hapo jambo ambalo lilimfanya azuie baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yakipangwa kufanyika bila kushikishwa kwa kamati yake hali iliyopelekea mwalimu mkuu wa shule hiyo kusimamia mwenyewe shughuli mbalimbali kama vile ujenzi wa vyoo katika shule hiyo.

Sekta ya elimu katika mkoa wa Shinyanga inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo migogoro ya hapa na pale kati ya uongozi wa shule na kamati za shule ambazo  kimsingi hupewa dhamana ya kusimamia shughuli za maendeleo ya shule husika.

Mfano hai  wa migogoro hiyo tunaushuhudia katika manispaa ya Shinyanga hususani katika Shule ya msingi Bugoyi B  ambako kumekuwa na mvutano wa chini chini kati ya uongozi wa shule hio na kamati ya shule.

Na katika hali ya kuwekana wazi leo mbele ya diwani wa kata hiyo ambaye pia ni naibu meya wa manispaa ya Shinyanga David Nkulila imeelezwa kuwa  mgogoro huo kati ya uongozi wa shule ya msingi bugoi B iliyopo katika manispaa ya Shinyanga na  kamati ya shule hiyo unatokana na kutoshirikishwa kwa kamati ya shule katika shughuli za maendeleo katika shule hiyo.

Hayo yamebainika leo  katika kikao  cha dharura cha kamati ya maendeleo ya kata ya ndembezi  kilichofanyika katika ofisi ya kata hiyo, kilichokuwa  na lengo la kutafuta ufumbuzi wa  mgogoro unaosababishwa na mapato ya shule yanayokusanywa kutoka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.

Akiongea katika kikao hicho cha dharura mwenyekiti wa kamati ya shule   Hosea Mbusule amesema  kamati yake haikuwa ikishirikishwa ipasavyo katika masuala ya maendeleo shuleni hapo jambo ambalo lilimfanya kuzuia baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yakipangwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kusitisha malipo ya  ujenzi wa choo.

Mbusule  pia amesema kamati yake imezuia  upikwaji wa  uji kwa ajili ya wanafunzi kwa kuwa baadhi yao hawakuwa wanapatiwa uji kwa kigezo cha  kutochangia pesa wakati mahindi yalitolewa kwa ajili ya wanafunzi wote .

Mwenyekiti huyo wa kamati ya shule  ameelezea wasiwasi wake kuwa huenda shilingi laki tisa ambazo zilikuwa zikikusanywa na wananchi kwa ajili ya maendeleo ya shule hiyo zikawa zimehujumiwa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni diwani wa kata ya ndembezi David Nkulila ameahidi  kumwita mkaguzi wa mahesabu wa ndani kutoka halmashauri ya manispaa ya Shinyanga ili kukagua matumizi na mapato katika shule hiyo ili kubaini kama kuna ubadhilifu umefanyika.

Stori /picha na Steve Kanyefu


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post