DINI YA AJABU YAIBUKA KIGOMA,YAKAZA WATU KWENDA SHULE NA HOSPITALI

Dini mpya iitwayo Matengenezo inayozuia waumini wake kwenda sekondari na  hospitali, imeingia wilayani Kakonko mkoani Kigoma.

Inakataza waumini wasiende sekondari na hospitali, kwa madai kuwa Biblia inawakataza kufanya hivyo.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Peter Toima  alibaini hayo juzi katika Kijiji cha Rumashi Kata ya Nyabibuye wilayani humo.

Alikuwa kwenye ziara katika shule za sekondari za wilaya hiyo mpya, ambapo kwanza  aligundua wanafunzi wengi hawajaripoti shuleni kuanza Kidato cha Kwanza.

Toima alipohoji kulikoni hawajaripoti katika shule walizopangiwa huku wale walioandikishwa darasa la kwanza, pia nao hawaripoti, alielezwa kuwa sababu za kiimani zinazokataza wengine kusoma.

Mkuu huyo wa Wilaya alikatiza ziara yake na kuanza msako wa kuwasaka wanafunzi hao ambao hawajaripoti shuleni pamoja na waumini wa dini hiyo ya Matengenezo.

Alisema aliamua kufanya hivyo, kwa sababu dini hiyo inawakosesha watoto haki yao ya msingi na kukiuka sheria za nchi, kwani ni haki ya kila mtoto kupata elimu.

Katika msako huo,  aliongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo na watendaji wa Halmashauri wakiwemo Maofisa Elimu Msingi na Sekondari. 

Viongozi hao walifika katika familia ya Mchungaji wa Kanisa la Matengenezo,  Medad Laurent (40). Baada ya kufika hapo, Toima  aliwakuta mabinti watatu waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka huu lakini hawajaenda, kutokana na kile Mchungaji huyo alichodai kuwa sekondari wanafundisha uongo, kinyume na maandiko matakatifu yanavyosema.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya aliamuru Mchungaji huyo na mabinti zake wawili, kushikiliwa na Jeshi la Polisi huku utaratibu wa kuwapeleka mabinti hao shule ukiendelea. Pia, aliamuru Mchungaji huyo kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za elimu.

Siku iliyofuata Toima na Kamati ya Ulinzi na Usalama, walifanya kikao na kukubaliana kuwapeleka mabinti hao, Naomi Medard (16) na Anastazia Medard (14) katika shule za sekondari zenye mabweni kwa kuwatenganisha ili wasiendelee kusambaza sumu ya kukataa shule. Naomi alipelekwa Shule ya Sekondari Nyamtukuza na Anastazia  Shule ya Sekondari Kanyonza.

Hata hivyo,  katika familia hiyo binti mmoja Beatrice Merdad (19) alibaki nyumbani kwa madai kuwa hakuchaguliwa kuendelea na Kidato cha Kwanza. Alidai kuwa hata angechaguliwa, asingeweza kuendelea kwani wanafundisha uongo na siku akifa hatakuwa na la kwenda kumwambia Muumba wake, kutokana na elimu hiyo ya dunia kuwapotosha.
Katika familia hiyo ya watoto saba,  wawili walifariki dunia kutokana na kutokwenda hospitali. 
 
Mama wa watoto hao, Julitha Sebastian (39) alipohojiwa baada ya mtoto wake mchanga kuonekana kudhoofika na nywele kubadilika rangi, alisema kuwa dini yao haiwaruhusu kwenda hospitali.

Alisema hakuwahi kumpatia mtoto huyo chanjo ya aina yoyote wala hakuwahi kujifungulia hospitali. 
 
Kuhusu watoto wake waliokufa, alisema Biblia inasema “Ni heri wafao katika Bwana”.

Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya hiyo, Florida Gandye alisema waumini wa kanisa hilo, awali walikuwa Wakristo Wasabato, kisha wakajiengua na kuanzisha dini hiyo yenye imani za ajabu.
 
Credit-ziro99blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post