WATUMISHI WA HALMASHAURI WALAZIMISHWA KUKOPA PIKIPIKI SHINYANGA

Katikati aliyevaa nguo nyeusi ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Mohamed Kiyungi -PICHA KUTOKA MAKTABA YA MALUNDE1 BLOG
Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imedaiwa kuwalazimisha watumishi wake kukopa pikipiki kwa lazima bila kujali hata kama mtumishi husika anayo yake binafsi hali ambayo imezua maswali mengi kwa watumishi wake ambao wamedai huenda pikipiki hizo zimepelekwa na kigogo mmoja ziuzike chap chap.

Wakizungumza na waandishi wa habari  mjini Shinyanga kwa sharti la kutotajwa majina yao baadhi ya watumishi hao  wamesema wameshitushwa na kitendo cha mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya wilaya, Mohamed Kiyungi kulazimisha mikopo hiyo hata kama mtu hahitaji kukopa ambapo agizo hilo  la mkurugenzi linawataka wakope pikipiki kwa lazima, ambapo kila mwezi kutakatwa shilingi elfu hamsini.

Watumishi hao wamedai kuwa pamoja na kukopeshwa kwa nguvu pikipiki hizo hakuna hata mmoja aliyekabidhiwa nakala ya mkataba wa ukopaji huo ambapo nakala zote zimebaki mkononi mwa mkurugenzi hali ambayo wanaitilia shaka huenda zimetolewa na serikali kwa ajili ya kusambazwa kwa watumishi wake bure.

Hata hivyo  mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Mohamed Kiyungi alipotafutwa na waandishi wa habari alikiri watumishi kutakiwa kukopa pikipiki hizo na kwamba lengo ni kutaka kuhakikisha wanawajibika kikamilifu katika utendaji kazi wao wa kila siku.


Aidha amesema ofisi yake imetoa maelekezo pikipiki hizo zitumike kwa shughuli za kiofisi tu badala ya shughuli binafsi kwa vile kila mwezi watendaji hao wa kata watakuwa wakilipwa fedha za kununulia mafuta lita 10 na kwamba siyo rahisi kwa mafuta hayo kutumika katika vyombo binafsi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post