WATENDAJI WA SERIKALI WAKIWEMO WABUNGE WATAJWA KUSHIRIKIANA NA WAGENI KATIKA VITENDO VYA UJANGIRI NCHINI TANZANIA



Khamis Mgeja
 
Mwenyekiti wa taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation ambaye pia ni mwenyekiti wa ccm mkoa wa Shinyanga  Khamis Mgeja  ameitahadharisha serikali  kuwa makini na wageni wanaokuja nchini kwa gia ya uwekezaji kutokana na kwamba wengi wao si wema wanajihusisha na vitendo viovu kama vile ujangiri wa nyara za serikali na utoroshaji wa madini nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana  mjini Arusha Mgeja ambaye taasisi yake inajishughulisha na masuala ya haki za binadamu,utawala bora,utamaduni na mila na desturi alisema kuna wageni ambao wamekuwa wakijihusisha na  vitendo vya ujangiri wakishirikiana na vigogo wa serikali hapa nchini wakiwemo wabunge na watendaji waliopewa dhamana ya usimamizi wa mali hizo.

Amesema taasisi yake ya Mzalendo imebaini kuwa wageni hao hawafanyi
matukio hayo peke yao bali wanashirikiana na watanzania ambao wamekosa
uzalendo wa nchi hii  kufanya ujangiri wa nyara za serikali, kukithiri kwa usafirishaji wa madawa ya kulevya na utoroshaji wa madini nje ya nchi hivyo kuiomba serikali kuwa mwangalifu kwa wageni hao ambao wengi wao wanakuja wakiwa na malengo mabaya kwa nchi hii.

Mgeja alisema  kutokana na uzembe wa watendaji wa serikali kuna
wageni pia wamekua wakikwepa kulipa hata  kodi kwa visingizio vya kufilisika kwa mitaji ya makampuni yao hali ambayo inazidi kulididimiza taifa la Tanzania.

 Mgeja ameishauri serikali kuutangaza mwaka huu  wa 2014 kama mwaka wa kuamsha uzalendo kwa watanzania na kuendesha vipindi maalum katika vyombo vya habari,matamasha kila wilaya ili kurejesha uzalendo kwa wananchi ambao unazidi kupotea kila kukicha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post