Hofu imetanda kwa waendesha pikipiki maarufu bodaboda na jamii kwa ujumla kufuatia mauaji ya kutisha
ya waendesha pikipiki ambao wameuawa kikatili kwa kuchomwa na vitu vyenye ncha
kali katika vichwa vyao na watu wanaodaiwa kuwa wateja wao.
Tukio la kwanza limetokea katika eneo la Bushushu kata ya
Ngokolo katika manispaa ya Shinyanga saa mbili asubuhi ambapo Iddy Omari (27) mwendesha pikipiki mkazi wa
mtaa wa Lumumba mjini Shinyanga aligundulika kuuawa kwa kuchomwa na kitu chenye
ncha kali kichwani upande wa kushoto na mbinu iliyotumika ni mtu huyo
asiyefahamika aliyejifanya mteja na kumkodi mwendesha bodaboda Desemba 29 mwaka 2013 kwenda eneo la Bushushu
alikokutwa ameuawa.
tukio la pili limetokea Desemba 30 mwaka 2013 katika eneo la
Mbugani kijiji cha Gembe kata ya Kagongwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga
ambapo majira ya saa moja asubuhi mwendesha pikipiki aitwaye Gwambo Laurent
(27) aligundulika akiwa ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali mara tatu
kichwani na watu wanaodaiwa kuwa ni wanyang’anyi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Evarist Mangala amesema
katika matukio yote mawili waendesha pikipiki hao wawili yametokea Desemba 30 mwaka 2013 na walinyang’anywa
pikipiki zao na amewataka waendesha pikipiki kuchukua tahadhari za kiusalama
pindi wanapokuwa kazini nyakati za usiku.