Inasikitisha!!! MWANDISHI WA HABARI ATEKETEA KWA MOTO NDANI YA NYUMBA,YADAIWA MOTO ULITOKANA NA MSHUMAA ULIOKUWA JUU YA KOCHI -KAHAMA

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa shinyanga ACP Kihenya Kihenya
Watu wawili akiwemo mwandishi wa habari Mazingira Fm iliyoko Bunda mkoani Mara wamekufa baada ya kuteketea na moto wakiwa wamelala chumbani kutokana na moto unasadikiwa kuwa  unatokana na mshumaa katika mtaa wa Shunu,kata ya Nyahanga wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa ya kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Kihenya Kihenya kwa vyombo vya habari tukio hilo limetokea jana saa tano usiku  katika mtaa wa Shunu mjini Kahama katika nyumba ya Christina Deus(38) mkazi wa mtaa huo.

Amewataja watu waliofariki dunia  kuwa ni Happiness Amos (24) mkazi wa Shunu mjini Kahama ambaye ni mwandishi wa habari wa Radio Mazingira iliyoko Bunda Mkoani Mara na Mariam Juma (2) ambaye pia ni mkazi wa mtaa huo.

Kamanda Kihenya amesema mbali na moto huo kusababisha vifo vya watu wawili pia watu wengine wawili walijeruhiwa ambao ni Alfred Alphonce (15) aliyejeruhiwa mkono wa kushoto pamoja na mmiliki wa nyumba hiyo Christina Deus (38) ambaye aliungua mikono yote miwili na mguu wake wa kushoto.

Amesema chanzo cha moto huo inasadikiwa kuwa ni mshumaa uliowashwa na kuwekwa juu ya kochi na kusababisha kuunguza nyumba huku akiongeza kuwa thamani ya mali iliyoteketea bado haijajulikana na kuongeza kuwa majeruhi waliokuwa ndani ya nyumba  hiyo wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na hali zao ni mbaya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments