MAPANGA TENA SHINYANGA-BALOZI WA MBUYUNI AKATWA MAPANGA KATIKA DARAJA LA MHUMBU


Balozi wa mtaa wa Mbuyuni uliopo kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga Pius Makonda amenusurika kufa baada ya kukatwa panga kisogoni na sehemu zingine za mwili wake na watu wasiojulikana kisha kunyang'anywa mali zake katika Daraja la Mhumbu lililopo katika barabara itokayo Shinyanga hadi Mwanza.hapa anaonesha sehemu aliyokatwa panga

Balozi wa mtaa wa Mbuyuniambaye pia ni Katibu wa Chama cha Wapanda Baiskeli mkoa wa Shinyanga (CHABASHI)
 
 
Akizungumza na malunde1.blogspot.com nyumbani kwake muda mchache baada ya kutoka hospitali ya mkoa wa shinyanga kupatiwa matibabu  Balozi huyo wa mtaa wa Mbuyuni ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Wapanda Baiskeli mkoa wa Shinyanga (CHABASHI)  alisema tukio hilo limetokea usiku  wa kuamkia leo majira ya saa nne wakati  akielekea nyumbani kwake akitokea mkoani Simiyu kikazi.

 Ameongeza kuwa  gari alilokuwa anasafiri nalo lilimshusha njiani,na hakupata tena usafiri ndipo akaanza kutembea kwa miguu na alipofika eneo la daraja  la Mhumbu  barabara ya Shinyanga-Mwanza kwenye matuta ya barabara akavamiwa na vibaka watatu waliokuwa na marungu na mapanga.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mbuyuni Chifu Abdallah Sube alisema matukio ya watu kukatwa mapanga yanazidi kuongezeka  na imefikia wakati wananchi wanaogopa kupita  kwenye baadhi ya maeneo kuanzia saa mbili usiku kwa hofu ya kukatwa mapanga.

Alisema hadi sasa hapo  katika daraja la Mhumbu watu zaidi ya wanne wakiwemo waendesha baiskeli maarufu daladala wamekatwa mapanga na watu wasiojulikana na kuporwa mali zao hivyo ameliomba jeshi la polisi kushirikiana na wananchi ili kuwabaini wahalifu.

Kwa upande wake kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Kihenya Kihenya alisema jeshi limeanza kufanya msako mkali  wa kubaini waharifu wakiwemo wanaojihusisha na mauaji mkoani  shinyanga ambapo jana waliwakamata watu watatu wakimiliki silaha kinyume cha sheria.
 Waliokamatwa ni Musa Mwendo (44) akiwa na bunduki aina ya shotgun yenye namba 85864 ikiwa na risasi moja,mkazi wa Bugomba A wilayani Kahama,Andrew Misana (30) Mkazi wa Bugomba B wilayani humo akiwa na bunduki aina ya gobore ikiwa na risasi zake yaani  goroli au malisau 30 pamoja na Melewa Bugarama(34) mkazi wa Bugamba B,akiwa na magobore mawili na malisau 45.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post