JKT kutangaza vijana 5,000 watakaojiunga kwa mujibu wa sheria

JESHI la Kujenga Taifa (JKT), wiki ijayo litatangaza majina ya vijana 5,000 waliohitimu kidato cha sita watakaojiunga na jeshi hilo kwa mujibu wa sheria kuanzia Machi, mwaka huu.

Huo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha aliyoitoa wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara yake, Julai 2012 bungeni Dodoma.
Alisema mafunzo hayo yamerejeshwa na yataanza kwa vijana wa Tanzania watakaomaliza kidato cha sita. Utaratibu wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria ulisimamishwa tangu mwaka 1994.

Baadhi ya vijana jana walionekana wakiwa Makao Makuu ya JKT, Mlalakuwa Dar es Salaam, wakitaka kufahamu kama wamechaguliwa kujiunga na jeshi hilo.

Hata hivyo, ofisa mmoja mwandamizi wa JKT ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema majina ya vijana hao yatatangazwa kuanzia wiki ijayo kwenye vyombo mbalimbali vya habari.
“Wasiwe na wasiwasi wiki ijayo kila kitu kitajulikana, majina ya waliochaguliwa yatatangazwa katika vyombo vya habari,” alisema.

Jarida la Vijana Leo Toleo la Novemba 2012, linalochapishwa na JKT, lilimkariri Waziri Nahodha akisema vijana watakaochaguliwa kujiunga na jeshi hilo wangetangazwa Januari, mwaka huu.
Alisema kambi za JKT zina uwezo wa kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja lakini kutokana na ufinyu wa bajeti wataanza kwa majaribio na vijana 5,000.

Jarida hilo lilimkariri Waziri Nahodha akisema wanafunzi 41,348 wanatarajiwa kuhitimu kidato cha sita mwaka huu na kwamba vilikuwa vikiandaliwa vigezo ili kuwapata vijana 5,000 wa kujiunga na JKT.

Kwa mujibu wa jarida hilo, mafunzo hayo yatakuwa ya miezi sita na yataendeshwa katika kambi za JKT Bulombora na Kanembwa mkoani Kigoma, Mlale mkoani Ruvuma, Mafinga mkoani Iringa, Msange Tabora na Oljoro mkoani Arusha.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alithibitisha kwa simu jana kuwa vijana 5,000 waliochaguliwa kujiunga na JKT kwa mujibu wa sheria watatangazwa wakati wowote kuanzia sasa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post