TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MTIHANI WA TAIFA WA KIDATO CHA PILI MWAKA 20121.0 Utangulizi
Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili mwaka 2012 unatarajiwa kufanyika nchini kote kuanzia tarehe 05/11/2012 na kumalizika tarehe 16/11/2012. Idadi ya shule/vituo vilivyosajili watahiniwa mwaka 2012 ni 4,242 ikiwa ni ongezeko la vituo 55 ikilinganishwa na vile vilivyosajiliwa mwaka 2011 ambavyo vilikuwa 4,187. Kwa hiyo kwa mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 1.3.
2.0 Watahiniwa
Jumla ya watahiniwa 442,925 wamejiandikisha kufanya mtihani. Kati yao wasichana ni 214,325 (sawa na asilimia 48.39) na wavulana ni 228,600 (sawa na asilimia 51.61). 
3.0 Umuhimu wa Mtihani wa Kidato cha Pili
Mtihani wa Kidato cha Pili kama ilivyo mitihani mingine ya taifa ni muhimu sana. Matokeo ya mtihani huu hutumiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania kama sehemu ya matokeo katika mtihani wa taifa wa elimu ya sekondari kidato cha nne. Mwaka huu, 2012 matokeo ya mtihani huu pia yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Aidha, mtahiniwa ataruhusiwa kukariri Kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi. 
4.0 Hitimisho
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaagiza Wadau wote wa Elimu katika Kanda, Manispaa na Halmashauri za Wilaya pamoja na Wazazi kuhakikisha kuwa wanafunzi wote walioandikishwa kufanya mtihani wanafanya bila kukosa.
Aidha, Wazazi, Walezi, Walimu na jamii kwa ujumla wanashauriwa kuwaandaa vema wanafunzi ili kuepukana na udanganyifu ikiwa ni pamoja na kuzingatia taratibu na sheria za uendeshaji wa mitihani. 
Nawatakia watahiniwa wote wa Kidato cha pili mwaka huu mafanikio mema katika mitihani yao. 
Dkt.  Shukuru Jumanne Kawambwa (Mb)
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
04/11/2012

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post