MCHUNGAJI AUWA MWANAFUNZI-SHINYANGA

Mwanafunzi mmoja aitwaye Danga dwashi (7) aliyekuwa anasoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Mwaningi iliyopo katika Kijiji cha Mwaningi Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga ameuawa kwa kukatwa na panga shingoni na  Selemani Lugolola ambaye alikuwa mchungaji  wa ng’ombe hapo nyumbani kwao.

Walioshuhudia tukio hilo wamesema tukio hilo limetokea wakati mwanafunzi huyo na mchungaji wa ng’ombe wakiwa wamelala kwenye chumba kimoja.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Evarist Mangalla amesema tukio hilo limetokea Novemba 21 ,2012 majira ya saa nne na nusu katika kitongoji cha Isambiro,Kijiji cha Mwaningi Kata ya Bulige Tarafa ya Msalala Wilayani Kahama na kuongeza kuwa chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.

Aidha mtuhumiwa  wa mauaji Selemani Lugolola alifanikiwa kutoroka baada ya kufanya mauaji hayo na anaendelea kutafutwa na jeshi la polisi kwa kushirikana na wadau mbalimbali ili afikishwe katika vyombo vya sheria.

Kamanda Mangalla ametoa wito kwa wananchi kuwa na tabia ya kuwafahamu vizuri watu wanaowaajiri ili inapotokea tatizo iwe rahisi kuwapata.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post