VIONGOZI WA UAMUSHO WANYOLEWA NDEVU ZAO

VIONGOZI wanane wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), akiwamo Sheikh Farid Hadi Ahmed jana walifikishwa mahakamani kwa mara ya pili, huku wakiwa wamenyolewa ndevu zao.
Sheikh Farid na viongozi wenzake walifikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa polisi na kufunguliwa mashtaka mawili.
Wakati wanafikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 22 mwaka huu  washtakiwa wote walikuwa na ndevu nyingi videvuni mwao, lakini jana walikuwa wamenyolewa na kuwafanya wawe na mwonekano tofauti jambo ambalo lililozua gumzo kubwa miongoni mwa watu waliofika kusikiliza kesi hiyo.
Awali, viongozi hao walitarajiwa kufikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwereke, badala yake walipelekwa Mahakama Kuu, Vuga mjini hapa na kufunguliwa mashtaka mapya.

Akiwasomea mashtaka watuhumiwa hao mbele ya Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar, George Kazi, Wakili wa Serikali, Raya Msellem alisema vitendo walivyofanya vinahatarisha amani Zanzibar, likiwamo tukio la Sheikh Farid Hadi Ahmed kutoweka hivi karibuni ambalo lilisababisha kuibuka ghasia kubwa visiwani humo.

Wengine waliofikishwa jana mahakamani ni masheikh Msellem Ali Msellem, Mussa Juma Issa, Azzan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman na Ghalib Ahmada Omar.

Wakili huyo alidai kuwa kuanzia Oktoba 17 hadi Oktoba 18, mwaka huu katika barabara kadhaa za Mkoa wa Mjini Magharibi washtakiwa hao walichochea wafuasi wao kuharibu barabara, kuvunja nyumba, kuharibu vyombo vya moto na kusababisha hasara ya Sh500 milioni.

Vilevile, Msellem alidai kuwa Mei 26 hadi Oktoba 19, mwaka huu katika maandamano yaliyofanyika Lumumba, Msumbiji, Fuoni Meli sita na Mbuyuni Unguja watuhumiwa wanadaiwa kuwashawishi watu wengine ambao hawapo kortini kufanya ghasia na kuhatarisha amani.
Baada ya mashtaka hayo, watuhumiwa hao walirudishwa tena Mahakama ya Mwanakwereke kuendelea na kesi yao ya awali. Hata hivyo, kesi hiyo haikuweza kusikilizwa kwa kuwa hakimu anayeisikiliza  hakuwapo mahakamani.

Washtakiwa hao wamerudishwa rumande hadi Novemba 7 kesi yao ya Mwanakwerekwe itakaposikilizwa na Novemba 8 wanatarajiwa kupanda tena kizimbani katika Mahakama Kuu kuendelea kusikiliza kesi yao.

Hata hivyo, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani bila ya kuwa na mawakili wao, Salim Tawfik na Abdallah Juma ambao wamejitoa katika kesi hiyo kwa madai ya kuwa wateja wao wanadhalilishwa.

Mawakili wajitoa
Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Vuga, mawakili hao walisema kitendo cha Serikali kuwashikilia wateja wao na kushindwa kuwaleta mahakamani ni dalili tosha ya kuonyesha haki haiwezi kutendeka, kwani ni kitendo kinachokwenda kinyume na sheria za kimataifa na sheria za nchi kwamba dhamana ni haki ya kila raia.
“Inaonyesha hapa haki haiwezi kutendeka, dalili zimeanza kuonyesha mapema kwa sababu kwanza wamezuiliwa kupewa dhamana wakati pande zote mbili hazikuwa na pingamizi la kutoa dhamana, lakini mahakama ndiyo inakataa kutoa dhamana,”alisema Salim Tawfik.

Tawfik alisema jambo lingine la kushangaza ni kwamba washtakiwa walitakiwa kufikishwa Mahakama ya Mwanakwerekwe, lakini baadaye wakaambiwa wateja  wao wamepelekwa Mahakama Kuu ya Vuga na kwamba walipofika huko hawakuwakuta maofisa wa mahakama.

“ Tunajitoa katika hii kesi kwa leo (jana) ili kufikisha ujumbe kwa Serikali kwamba hawawatendei haki wateja wetu,” alisema.

Jumatatu iliyopita watu saba bila kuwamo Ghalib Ahmada Omar walifikishwa katika Mahakama ya Mwanakwerekwe kwa madai ya kufanya uchochezi katika mhadhara uliofanyika Agosti 17 mwaka huu.

CUF yataka Sheikh Ponda aachiwe
Mwenyekiti wa Chama cha  Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba amesema ili kuinusuru nchi isiingie katika mgogoro ni vyema Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake wapewe dhamana.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Lipumba alisema maelezo yaliyotolewa na polisi ya kumhusisha Sheikh Ponda na vurugu hizo hayana ushahidi wowote bali yanaongeza mfarakano katika jamii.

“Unaweza usikubaliane na Sheikh Ponda katika maelezo na msimamo wake kuhusu dhuluma dhidi ya Waislamu,  lakini ni makosa kumsingizia mambo ambayo hakuyatenda,”alisema.

Profesa Lipumba alisema hata kesi aliyoshtakiwa Sheikh Ponda ni ya kuvamia kiwanja kisichokuwa chake kilichokuwa kinamilikiwa na East African Muslim Welfare Society kwa madhumuni ya kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu na kwamba kesi hiyo ni ya Mahakama ya Ardhi.

Alisema anachodai Sheikh Ponda ni kuwa kiwanja hicho cha Waislamu kimeuzwa kinyume na utaratibu na sheria zinazolinda mali ya Waqfu.

Lipumba alisema mwenye kiwanja alistahili kwenda Mahakama ya Ardhi na kueleza kuwa kiwanja chake kimevamiwa, hivyo kutumia polisi kumkamata Sheikh Ponda kumechochea vurugu hizo.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, matamshi ya Kamanda Kova ya kumuhusisha Sheikh Ponda na uchomaji wa makanisa jambo ambalo hakuhusika nalo na kutoa wito kwa wafuasi wa Sheikh huyo kujisalimisha polisi ndiko kulikochochea maandamano ya Ijumaa iliyopita.

Alisema kitendo cha kuwaingiza barabarani askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupambana na raia ni kitendo cha aibu na cha kusikitisha kwani kazi ya wanajeshi ni  kulinda mipaka na siyo kwenda kupiga raia wanaoandamana.

Lipumba aliitaka Serikali iepuke kujenga uhasama kati ya Jeshi la Wananchi na raia.

CUF pia imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za kuleta maelewano ya kujenga utamaduni wa kuvumiliana baina ya Watanzania wenye imani tofauti.

Waislamu watoa tamko
Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, umeitaka Serikali kuwaachia Waislamu wote waliowekwa ndani kwa tuhuma zilizotokana na vurugu ambazo zilisababishwa na mtoto aliyekojolea Quran.

Pia wanazuoni hao wameitaka Serikali kuitisha kikao cha pamoja baina ya viongozi wa taasisi zote za Kiislamu na wale wa Kikristo kuzungumzia uhusiano baina ya wafuasi wa dini hizo mbili unaozidi kuzorota.

Akisoma tamko hilo, Sheikh Yasin Kachechele  alisema vurugu hizo zilisababishwa na uzembe wa wazazi, viongozi wa mtaa na hata vyombo vya dola kutokana na kuchelewa kuchukua hatua stahiki.

"Kuachiliwa kwa Waislamu hawa kutarejesha utulivu kwa kiasi kikubwa na kuruhusu hatua za kuganga majeraha ziende kwa mioyo mikunjufu," alisema Kachechele.


Haki za Binadamu wataka Tume huru
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Zanzibar, imeishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuunda tume huru kuchunguza madai ya kutekwa kwa Kiongozi wa Jumuiya za Kiislamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed hivi karibuni.

Kiongozi huyo alitekwa Oktoba 16 kabla ya kuonekana siku tatu baadaye, huku akisisitiza kuwa polisi ndiyo waliomteka.

“Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaishauri Serikali kuunda Tume huru kuchunguza dai hili kwa kina na hatimaye kutoa ripoti kwa wananchi,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa jana mjini hapa.

Baada ya kuibuka, Sheikh Farid alidai kuwa alitekwa na vyombo vya dola lakini Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa lilikanusha madai hayo.

Kutoweka kwa Sheikh Farid, Oktoba 16 usiku kulifuatiwa na vurugu za wafuasi wa Jumuiya ya kidini ya Uamsho kwa siku tatu kuanzia Oktoba 17 na polisi kulazimika kutumia nguvu za ziada kuzima vurugu hizo kwa kufyatua mabomu ya machozi na risasi za moto.

Tume hiyo pia imelaani kitendo cha kuuawa kwa polisi Said Abdulrhaman ikieleza kuwa kitendo hicho ni kupingana na haki za binadamu na kinapingana na sheria za nchi na kinyume cha Katiba.
Imeandaliwa na Masoud Sanani na Salma Said (Zanzibar), Nora Damian na Boniface Meena (Dar).

SOURCE: MWANANCHI.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments