TAARIFA KWA UMMA KUTOKA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII:TAHADHARI YA UGONJWA WA MARBURG




TAHADHARI YA UGONJWA WA MARBURG


Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii
, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani
(WHO), tarehe 20 Oktoba, 2012 kuhusu ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza
katika nchi jirani ya Uganda. Maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni
Wilaya ya Kabale, Kanda ya Kusini Magharibi ya nchi, na wilaya hii inapakana
na Rwanda. Mpaka tarehe 24 Oktoba 2012, takriban watu 13 wamepata maambukizo
na 6 wamepoteza maisha..


Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania
na hasa wale waliopo katika mikoa ambayo inapakana na na nchi jirani
ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Kigoma).


Marburg ni
ugonjwa wa hatari unaofanana na Ebola na unasababishwa na virusi vijulikanavyo
kwa lugha ya kitaalam “Marburg Virus”. Ugonjwa huu ni miongoni mwa
magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za Virusi zinazosababisha
kutokwa damu mwilini, (Viral Haemorrhagic Fevers). Chanzo kamili cha
virusi vya ugonjwa huu hakijulikani. Hali inayosababisha mlipuko wake
pia haijulikani. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.


Dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na Homa kali, inayoambatana
na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia ya haja
kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali inayopelekea kifo
kwa muda mfupi.


 Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.


Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na haraka kutoka
mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana
na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili, ikiwa
ni pamoja na jasho au kumgusa  mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg.Ugonjwa
huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa
wa Marburg.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua
zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:

  • Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia
    kwa Waganga Waku
    u wote wa Mikoa na Wilaya. Aidha taarifa hii
    pia
    imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la
    Ugonjwa),  “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa
    namna
    ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.    



  • Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu
    wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia
    wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa
    huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.
  • Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi
    wa afya

Wananchi wanashauriwa kutokuwa
na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa nchini.
Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya
kilicho karibu mara watakapoo
na mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za
ugonjwa huu.

Kitengo cha mawasiliano ya Serikali


25/10/2012

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments