Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAWAKE 60 WANUFAIKA NA UFADHILI WA MASOMO KUPITIA WISE


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Wanawake 60 wamefanikiwa kunufaika na ufadhili wa masomo kupitia programu ya Women in Sustainable Energy (WISE), tangu ilipoanzishwa mwaka 2023, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza ushiriki wa wanawake wenye ujuzi wa kitaalamu katika sekta ya nishati nchini.

Wanufaika hao ni pamoja na wanawake 15 wa kundi la nne la programu hiyo, inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Serikali ya Ireland na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), kwa lengo la kujenga uwezo wa wanawake katika taaluma za nishati endelevu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Injinia Iman Mruma, amesema kundi hilo jipya linaongeza wanufaika 15 juu ya wanawake 45 waliopata ufadhili kupitia makundi matatu yaliyotangulia.

Amesema uwekezaji katika sekta ya nishati unapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya wataalamu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

“Sekta ya nishati ni mhimili wa mageuzi ya uchumi, ukuaji wa viwanda na maendeleo endelevu, hivyo uwekezaji katika miundombinu unapaswa kwenda sambamba na kujenga rasilimali watu yenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za sekta hiyo,” amesema.

Mruma amesema kuwawezesha wanawake kupata maarifa ya kiufundi si suala la usawa wa kijinsia pekee, bali pia ni uwekezaji wa kimkakati katika maendeleo ya uchumi na usalama wa nishati nchini.

Amezitaja fursa zinazozidi kuongezeka katika maeneo ya nishati jadidifu, matumizi bora ya nishati, nishati safi ya kupikia na usafiri unaotumia umeme, akiwataka wanufaika kutumia elimu watakayoipata kubuni suluhisho za changamoto za sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Shigeki Komatsubara, amesema Tanzania inahitaji kuongeza idadi ya wanawake wenye ujuzi wa kitaalamu ili washiriki kikamilifu katika kuongoza mageuzi ya nishati yanayolenga kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Amesema azma ya kujenga uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, huku idadi ya watu ikitarajiwa kuzidi milioni 118, inahitaji wataalamu wengi wa uhandisi, wabunifu na viongozi wenye uwezo wa kusukuma maendeleo.

Komatsubara amesema kabla ya kuanzishwa kwa programu ya WISE mwaka 2023, wastani wa wanawake wawili pekee walikuwa wakijiunga kila mwaka katika programu ya Shahada ya Uzamili ya Uhandisi wa Nishati Endelevu, hali iliyochochea kuanzishwa kwa mpango huo ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika taaluma hiyo.

Ameeleza kuwa kupitia programu hiyo, wanufaika hupata ufadhili wa masomo, mafunzo ya vitendo, vyeti vya kitaalamu na ushauri wa kitaaluma, huku baadhi ya wahitimu wakianza kufanya kazi katika maeneo ya ukaguzi na usimamizi wa matumizi ya nishati.

Aidha, amewahimiza wanufaika kutumia maarifa watakayopata kutafuta suluhisho la changamoto za nishati nchini, pamoja na kutembelea shule ili kuhamasisha wasichana wengine kuchagua taaluma za sayansi, teknolojia na uhandisi.

Naye Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan, amesema kuwawezesha wanawake katika elimu na ajira hakumaanishi kuwaondoa wanaume katika nafasi zao, bali ni kuhakikisha kila mmoja anapata fursa sawa ya kushiriki katika maendeleo ya taifa.

Amesema uzoefu wa Ireland unaonesha kuwa wanawake wana uwezo wa kushika nafasi za juu za uongozi wanapopewa fursa, akibainisha kuwa kwa sasa asilimia 55 ya mabalozi wa nchi hiyo ni wanawake.

Brennan pia amefichua kuwa asilimia 75 ya wanawake walionufaika na kundi la tatu la programu ya WISE wamefanikiwa kupata ajira kabla ya kuhitimu masomo yao.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya wanawake, huku akieleza kuwa lengo ni kuongeza idadi ya wanufaika wa programu hiyo kutoka 60 hadi 100 kwa haraka zaidi.

Akizungumzia manufaa ya programu hiyo, mmoja wa wanufaika, Athnaa Rashid, amesema WISE imemwezesha kupata zaidi ya ufadhili wa masomo, ikiwamo maarifa na uzoefu wa vitendo kupitia ziara katika miradi mbalimbali ya nishati nchini.

Amezitaja ziara katika mradi wa umeme wa jua wa Kishapu mkoani Shinyanga, vituo vya kuzalisha umeme kwa maji mkoani Morogoro, miradi ya upepo na maeneo ya utafiti wa nishati ya jotoardhi kuwa sehemu ya mafunzo yaliyomjengea uelewa wa vitendo.

Amesema uzoefu huo umemsaidia kuelewa namna rasilimali za nishati zinavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi kupitia huduma za afya, elimu, maendeleo ya vijijini na uzalishaji viwandani.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Nishati imesema itaendelea kushirikiana na UNDP, Serikali ya Ireland na DIT kuimarisha programu hiyo kwa kupanua fursa za mafunzo kwa vitendo, ziara za viwandani, ushauri wa kitaaluma na ajira kwa wanufaika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com