Na Sumai Salum-Kishapu
JUMLA ya wahitimu 40 wa mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, wamehitimu mafunzo yao katika mahafali ya pili yaliyofanyika Novemba 16, 2026, huku Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Lucy Mayenga, akiahidi kuwasomesha vijana 10 watakaojiunga na chuo hicho mwaka ujao.
Wahitimu hao wamepata mafunzo katika fani mbili, ambapo 20 wamehitimu fani ya umeme na wengine 20 fani ya ushonaji kwa kutumia cherehani, hatua inayolenga kuwawezesha vijana kujiajiri na kujipatia kipato kupitia ujuzi walioupata.
Akizungumza katika mahafali hayo akiwa mgeni rasmi, Mhe. Mayenga amewapongeza wahitimu na wazazi kwa kuthubutu kuwapeleka watoto wao katika mafunzo ya ufundi stadi, akieleza kuwa ufundi ni eneo lenye fursa kubwa za ajira na ujasiriamali ambalo linaweza kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Aidha, ameahidi kuwasomesha vijana 10 watakaoanza mafunzo mwaka ujao, huku akimtaka Mkuu wa Chuo hicho kuweka kanzidata ya wahitimu ili kurahisisha kuwaunganisha na wateja, taasisi za Serikali na watu binafsi wanaohitaji huduma zao. Pia ameahidi kuleta tenki kubwa la maji kusaidia chuo wakati wa uhaba wa maji na kuunga mkono juhudi za kuanzisha mafunzo ya uchomeleaji, huku akieleza kuwa fani ya ufundi mabomba itaendelea kufanyiwa kazi.
"Ninawataka vijana msiwe na haraka ya kukata tamaa, mwanzo huwa mgumu lakini uvumilivu, uaminifu na kujituma katika kazi zenu ni mambo muhimu. Mtangulize Mungu katika kazi zenu na mkafanye kazi kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa mkubwa huko uraiani,” amesema Mayenga.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kishapu, Tajiri Mollel, amesema chuo kinaendelea kukabiliana na mahitaji ya vifaa na zana za mafunzo, kuboresha miundombinu na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu ya ufundi stadi ili vijana wengi zaidi wanufaike na fursa zilizopo.
Mollel amewataka wahitimu kutumia ujuzi walioupata kwa vitendo, kudumisha nidhamu, uaminifu na heshima kwa wateja na waajiri, kutokata tamaa wanapotafuta ajira na badala yake kutumia maarifa yao kujiajiri. Pia amewasisitiza kuzingatia usalama kazini, viwango vya ubora na kuwa mabalozi wazuri wa chuo kwa kuonesha mfano kupitia kazi zao.
“Tunawashukuru Serikali, VETA, viongozi wa Wilaya, wadau wa maendeleo, wazazi na walezi kwa ushirikiano wao. Tutaendelea kujitoa kutoa mafunzo bora yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira na kukuza ujasiriamali kwa vijana,” amesema Mollel.
Wakizungumza kwa niaba ya wahitimu, wanafunzi hao wameishukuru Serikali kwa kuanzisha chuo hicho wilayani Kishapu, walimu kwa kuwapatia maarifa na ujuzi waliouhitaji, pamoja na wazazi na walezi kwa kuwaunga mkono katika safari yao ya mafunzo. Wamesema wako tayari kutumia ujuzi walioupata kujiajiri, kutoa huduma bora kwa jamii na kushiriki katika maendeleo ya Taifa.
Mahafali hayo yamekuwa sehemu ya kuonesha umuhimu wa elimu ya ufundi stadi katika kuwawezesha vijana kujitegemea, kupunguza utegemezi wa ajira za kuajiriwa na kuongeza idadi ya mafundi wenye ujuzi katika jamii.
Mwakilishi wa Wazazi akizungumza kwenye Mahafali hayo Samwel Daniel akizungumza kwa niaba ya wazazi kwenye mahafali hayo
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Shija Ntelezu akizungumza kwenye mahafali hayo
TAFUTA HABARI
Social Plugin