Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

USALAMA WA WAANDISHI WA HABARI NI WAJIBU WA KILA MMOJA-SOKO

Na Edwin Soko-Mwanza

Siku ya Kimataifa ya Kupinga Uhalifu Dhidi ya Waandishi wa Habari huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 2 Novemba.


Siku hii ilianzishwa na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuikumbusha dunia kuhusu umuhimu wa kulinda usalama wa waandishi wa habari na kuhakikisha kuwa wote wanaofanya uhalifu dhidi yao wanachukuliwa hatua za kisheria.


Historia ya siku hii inatokana na tukio la kusikitisha lililotokea nchini Mali, Afrika Magharibi, tarehe 2 Novemba 2013, ambapo waandishi wawili wa habari raia wa Ufaransa waliuawa wakiwa katika majukumu yao ya kikazi.


Waandishi hao walikuwa Ghislaine Dupont na Claude Verlon, waliokuwa wakifanyia kazi Shirika la Utangazaji la Ufaransa, Radio France Internationale (RFI).


Siku hiyo, waandishi hao walikuwa katika mji wa Kidal, kaskazini mwa Mali, wakitekeleza majukumu yao ya kihabari. Walikuwa wamekwenda kufanya mahojiano na viongozi wa kundi la waasi lililokuwa likifanya shughuli zake katika eneo hilo.


Baada ya kumaliza mahojiano, walitekwa na watu wenye silaha na kuuawa. Mauaji hayo yalizua mshtuko mkubwa duniani na kuibua mjadala kuhusu hatari zinazowakabili waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, hasa katika maeneo yenye migogoro na ukosefu wa usalama.


Uamuzi huo ulizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za makusudi katika kuzuia uhalifu dhidi ya waandishi wa habari, kufanya uchunguzi wa haraka na huru pale uhalifu unapotokea na kuwafikisha wahusika mahakamani ili wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwin Soko

Hatua ya Umoja wa Mataifa


Umoja wa Mataifa pia uliipa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) jukumu la kuratibu na kuhamasisha utekelezaji wa maadhimisho hayo duniani.


Maadhimisho ya kwanza ya siku hii yalifanyika mwaka 2014, yakiwa na lengo la kuunganisha serikali, taasisi za habari, mashirika ya kutetea haki za binadamu na wadau wengine katika kupambana na utamaduni wa kutoadhibiwa kwa wahusika wa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari

Kwa nini siku hii ni muhimu?


Siku hii ina umuhimu mkubwa kwa sababu inatukumbusha kuwa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari si suala linalowaathiri wanahabari pekee, bali ni tishio kwa haki ya jamii kupata taarifa na uhuru wa kujieleza.


Uhalifu huo unajumuisha mauaji, utekaji nyara, kupigwa, kuteswa, vitisho, kukamatwa kiholela, mashambulizi ya kimtandao na vitendo vya unyanyasaji vinavyolenga kuwazuia waandishi kutekeleza majukumu yao.


Mwaka 2026 umeendelea kushuhudia mauaji ya waandishi wa habari katika maeneo mbalimbali duniani, hususan katika maeneo yenye migogoro ya kivita na uhalifu uliopangwa.


Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ) iliyotolewa Oktoba 30, 2026, waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari 15 wameuawa duniani mwaka 2026 kutokana na kazi zao za kihabari.


Wito kwa serikali na wadau wa habari., Maadhimisho haya yanapaswa kuwa zaidi ya hotuba, mikutano na matamko.


Yanapaswa kuwa fursa ya kutathmini hatua zinazochukuliwa kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari na kuwawajibisha wale wote wanaohusika na uhalifu dhidi yao.


Serikali zinapaswa kuhakikisha mazingira salama ya kufanya kazi kwa waandishi wa habari,


Vyombo vya dola vinapaswa kuchunguza matukio ya ukiukwaji wa haki za wanahabari, na Mifumo ya mahakama inapaswa kuhakikisha haki inatendeka.


Kwa Afrika na Tanzania kwa ujumla, siku hii ni wito wa kuimarisha usalama wa wanahabari, kulinda uhuru wa habari na kujenga mazingira ambayo mwandishi anaweza kutekeleza wajibu wake bila hofu, vitisho au kushambuliwa.


Hapa Nchini Tanzania kumekuwa na juhudi mbalimbali za kushughulikia matukio ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari.


Ndugu waandishi wa habari wenzangu wakati tukifanya tafakuri juu ya maadhimisho haya nitoe wito kwenu kuwa, msingi wa kwanza wa usalama wetu ni kufanya kazi kwa kuzingatia weledi ili kupunguza uhasama na chuki.


Lakini pia kwa umoja wetu tuhimize kusema tunapopatwa na matukio ya ukatili wakati tukitimiza majukumu yetu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com