Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDEJEMBI AAGIZA USIMAMIZI MADHUBUTI WA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO


Na: OWM - TAMISEMI, Kigonsera - Mbinga

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amehimiza usimamizi madhubuti na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo zinazoelekezwa kwenye halmashauri zote na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, elimu na afya, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Novemba 11, 2026, akiwa Kigonsera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi na kuwapa fursa ya kupata ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya ya Mbinga, mkoani  Ruvuma.

“Mhe. Waziri wa TAMISEMI, kupitia Halmashauri zetu, hakikisha fedha zinazoletwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinasimamiwa kikamilifu na kuwe na uwajibikaji kwa watakaobainika kuzitumia tofauti na malengo,” amesisitiza Mhe. Ndejembi.

Akipokea maelekezo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameahidi kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa fedha za miradi, ikiwemo Shilingi Milioni 455 zilizoletwa Kigonsera kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa mita 800, ambapo kwa sasa mkandarasi yupo kazini.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amesema kuwa ofisi yake italeta Mbinga Shilingi Milioni 900 kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya, huku akiahidi kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri katika ukarabati wa hospitali hiyo ili  kutoa huduma bora kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com