HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imeendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia katika sekta ya afya kati ya Tanzania na Uingereza kupitia ushirikiano wa kimataifa na taasisi ya BAUS Urolink, unaolenga kuboresha huduma za kibingwa na kubadilishana utaalamu.
Hatua hiyo imedhihirika leo Novemba 16, 2026 jijini Mbeya, wakati Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali, Dkt. Godlove Mbwanji, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa madaktari bingwa kutoka taasisi BAUS ya Uingereza, mazungumzo yaliyokwenda sambamba na kuanza kwa kambi maalum ya matibabu na mafunzo ya mfumo wa mkojo (Urology).
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mbwanji amesema ushirikiano huo wa kimataifa ni matunda ya diplomasia imara inayofungua milango ya wataalamu wa kigeni kuja kushirikiana na madaktari wazawa wa mikoa ya Mbeya, Katavi, na Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla.
"Tunawashukuru na kuwapongeza kwa ushirikiano huu wenye tija. Niwasihi muendelee kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu ya Tanzania na hospitali yetu mnaporejea nchini kwenu au mnapotembelea mataifa mengine," alisema Dkt. Mbwanji.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Urolink, Dkt. Suzie Venn, ambaye ameambatana na mabingwa wenzake Dkt. Paul Anderson na Dkt. Stephen Griffin, ameushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa mapokezi mazuri yanayoakisi uhusiano mwema baina ya mataifa hayo mawili.
Dkt. Venn amepongeza maboresho makubwa ya miundombinu na vifaa tiba hospitalini hapo, akiahidi kuwa taasisi yake itaendeleza ushirikiano huo wa muda mrefu wa kubadilishana uzoefu na madaktari wazawa sambamba na kutoa huduma kwa watu wazima na watoto.







TAFUTA HABARI
Social Plugin