Na Mwandishi wetu, Mwanza
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameridhishwa na ubora wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini wenye thamani ya Shilingi bilioni 18.6 huku akiitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha asilimia 10 ya kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati ili bandari hiyo ianze kutoa huduma zilizokusudiwa.
Hayo yamesemwa Mkoani Mwanza na Profesa Mbarawa Mara baada ya Kukagua Maendeleo ya mradi huo ambapo amesema kuwa Hadi sasa Mradi huo umefikia Asilimia 90 ya utekelezaji.
"Nitoe Pongezi kwa ( TPA) kwa usimamizi mzuri wa mradi na ubora wa kazi zilizotekelezwa huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha kazi zilizobaki kwa wakati ili bandari hiyo ianze kutoa huduma na kuwanufaisha wananchi pamoja na wadau wa sekta ya usafirishaji. "Amesema Profesa Mbarawa."
Naye Mhandisi Dkt Baraka Mdima Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania (TPA) amesema kuwa mamlaka hiyo inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa.
Aidha maboresho yanayofanyika katika bandari hiyo yameongeza kina cha maji kutoka mita tatu hadi mita tano hatua ambayo itawezesha meli kubwa zaidi kutia nanga hivyo kuongeza uwezo wa bandari hiyo katika kuhudumia shehena.
Hata hivyo urefu wa gati umeongezeka kutoka mita 350 hadi mita 700 jambo ambalo litaongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli nyingi zaidi na kuboresha ufanisi wa huduma za usafirishaji katika Ziwa Victoria.
"Mradi wa ujenzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali katika kuboresha miundombinu ya bandari za Ziwa Victoria, kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo na abiria, pamoja na kuimarisha shughuli za usafirishaji na biashara katika ukanda huo. Amesema "Mhandisi Mdima".

TAFUTA HABARI
Social Plugin