Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KAPINGA ASHIRIKI UZINDUZI WA MJI WA SERIKALI MTUMBA


📌 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua majengo ya ofisi za Wizara, taasisi za Serikali na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba.

📌 Serikali imewekeza takribani Shilingi bilioni 700 katika ujenzi wa Mji huu ulioanza mwaka 2021.

📌 Mji wa Serikali una majengo ya Wizara 26, taasisi 11 za Serikali, taa 1,635, kilomita 57.1 za barabara za lami, kilomita 59.1 za njia za waenda kwa miguu na kilomita 59.1 za njia za waendesha baiskeli.

Dodoma

Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), ameshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026, uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa ameambatana na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço, aliyeshiriki kama mgeni maalumu, huku Rais Samia akiwa mgeni rasmi.

Uzinduzi huo ni sehemu ya hatua za Serikali katika kuimarisha shughuli za kiutawala na kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa Wizara na taasisi za umma, kufuatia uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali jijini Dodoma uliofikiwa mwaka 2016.

Serikali imewekeza takribani Shilingi bilioni 700 katika ujenzi wa Mji huo ulioanza mwaka 2021, unaojumuisha majengo ya ofisi za Wizara 26 na taasisi 11 za Serikali, pamoja na taa 1,635 za barabarani kwa ajili ya kuimarisha mwanga katika maeneo mbalimbali ya mji huo.

Katika upande wa miundombinu ya usafiri, Mji wa Serikali Mtumba una kilomita 57.1 za barabara za lami zinazotumiwa na magari, kilomita 59.1 za njia maalumu za waenda kwa miguu na kilomita 59.1 za njia za waendesha baiskeli, hatua inayowezesha matumizi ya njia tofauti kulingana na mahitaji ya watumiaji.

Aidha, barabara za Mji wa Serikali Mtumba zimepewa majina ya Marais waliowahi kuliongoza Taifa pamoja na barabara yenye jina la Rais wa sasa, ikiwa ni sehemu ya kutambua historia ya uongozi wa nchi.

Ushiriki wa Wizara ya Viwanda na Biashara katika hafla hii Uliwakilishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. judith Kapinga ambae aliambatana na Naibu Waziri Mhe Dennis Londo, Katibu Mkuu Balozi Waziri Rajab, Salum, Naibu Katibu Mkuu Aristides Mbwasi, Menejinenti ya Wizara ya Viwanda na  Biashara na wafanyakazi wa Wizara ya Viwanda na Biashara. 

Mji wa Serikali Mtumba unalenga kuimarisha uratibu na mawasiliano baina ya Wizara na taasisi za Serikali, kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.





















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com