DODOMA, Septemba 23, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kikwete, amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo kuhakikisha wataalamu wa utunzaji na usimamizi wa kumbukumbu wanapatiwa fursa za kuendelea na elimu na mafunzo zaidi, ikiwemo kupata elimu nje ya nchi.
Waziri Kikwete ametoa agizo hilo wakati akifungua Mkutano wa 14 wa TRAMPA, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwa na wataalamu wenye ujuzi, maarifa na uwezo unaoendana na mabadiliko ya teknolojia katika eneo la usimamizi na utunzaji wa kumbukumbu.
Amesema kuwa kumbukumbu ni sehemu muhimu ya historia na utendaji wa Serikali, hivyo kuna umuhimu wa kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wanaohusika na utunzaji, usimamizi na uhifadhi wa kumbukumbu.
Aidha, Waziri Kikwete amemtaka Katibu Mkuu kuhakikisha wataalamu hao wanapata fursa za kujifunza ndani na nje ya nchi ili kuongeza ujuzi na kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka mataifa mengine.
Ameeleza kuwa elimu na mafunzo hayo yatasaidia wataalamu kukabiliana na changamoto za kisasa, hususan katika matumizi ya teknolojia katika uhifadhi na usimamizi wa kumbukumbu.
Waziri Kikwete amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wataalamu kuendeleza taaluma zao, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kulinda kumbukumbu muhimu za Taifa.




Social Plugin