Na John Mapepele, WAF- New York
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Tanzania imepunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Ndejembi amesema haya leo wakati akihutubia Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81) akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan jijini New York, Marekani.
Amefafanua kuwa dhamira ya kisiasa ni muhimu sana katika kutekeleza uwekezaji unaolenga matokeo mahususi.
Amesema uzoefu unaonesha kuwa tunapowekeza katika miradi inayotekelezeka na kuweka wananchi kuwa kiini cha mipango hiyo maendeleo yanaweza kutoka katika ahadi na kuwa matokeo yanayoweza kupimika.
"Katika hilo, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto kwa kuongeza kiwango cha wanawake wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022" Amesema Mhe. Ndejembi.
Akiendelea kuhutubia mkutano huo Mhe. Ndejembi amesema ni katika misingi hiyo ambapo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alikubali jukumu la kuwa Kinara wa Afya ya Mama na Mtoto kwa Umoja wa Afrika.
Pia amesema kwa sasa dhamira Serikali ya Tanzania inalenga kusonga mbele katika kutekeleza ajenda ya “Three Zeros”, yaani malengo matatu ya kutokuwepo kwa vifo vya akina mama na watoto vinavyoweza kuzuilika, kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani, na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.
"Uzoefu wetu unaonesha kuwa hii ni ajenda ambayo Afrika inaweza kuifikia kwa mafanikio, lakini itahitaji uongozi wa kisiasa endelevu, upatikanaji wa fedha za kutosha na kuimarishwa kwa ushirikiano." ameongeza Mhe. Ndejembi
Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuungana na Tanzania katika kuipa ajenda hii msukumo mkubwa zaidi.
Awali, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika kikao cha 81 (UNGA
Waziri wa Afya Mhe.Mohamed Mchengerwa wakati akizungumza katika kikao cha ‘Sustaining Sierra Leone’s Triple Zero Gains Through 2028’, katika mjadala kuhusu namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana Sierra Leone katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuongeza huduma za chanjo alisisitiza kuwa Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mpango wa Umoja wa Afrika wa AU Champion Roadmap 2026–2030 unaolenga kufikia malengo ‘zero tatu’, ambayo ni kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani na usio na wataalamu, kutokuwepo kwa vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.
“Tanzania inajivunia kuwa na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika ajenda hii. Chini ya uongozi wake, tunaunga mkono kikamilifu AU Champion Roadmap 2026–2030 na Zero tatu,” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Katika mkutano wa mwaka huu wa UNGA 2026 mambo yanayojadiliwa ni pamoja na amani na usalama, vita na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, AI, afya ya dunia , maendeleo na SDGs.
Kaulimbiu ya UNGA 81 ni (Restoring Trust, Managing Transformation), Kurejesha Imani, Kusimamia Mabadiliko.




Social Plugin