
Na Regina Ndumbaro-Mbeya
Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni tisa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara ya TANZAM kutoka Nsalaga hadi Songwe mkoani Mbeya, huku utekelezaji wa mradi huo wa njia nne ukiwa umefikia asilimia 44.8.
Barabara hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilomita 29 inajengwa na TANROADS Mkoa wa Mbeya kwa lengo la kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo, kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu inayounganisha Tanzania na Zambia, pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi ndani ya nchi na mataifa jirani.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema fedha hizo zimewezesha mkandarasi kurejea eneo la mradi na kuendelea na utekelezaji wa ujenzi.
Amesema kwa sasa kazi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa madaraja, ikiwemo flyover katika eneo la Mafiati, pamoja na ujenzi wa barabara za chini (underpass) katika eneo la Kabwe na uboreshaji wa vivuko vya watembea kwa miguu katika maeneo maalum.
Aidha, amesema mradi huo utahusisha pia ujenzi wa madaraja ya Nzovwe na sehemu mbalimbali za kutembelea magari.
Mhandisi Bishanga amesema TANROADS Mkoa wa Mbeya inaendelea kuimarisha usimamizi wa miradi hiyo ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa na kuwaondolea wananchi changamoto ya vumbi na usafiri.
Ameongeza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha barabara nyingi za TANROADS Mkoa wa Mbeya zinawekwa lami, huku miradi mingine ikiwemo Daraja la Magufuli likiendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi jirani.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Mbeya, jambo linalotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa watu na mizigo, kufungua fursa za kiuchumi na kurahisisha biashara katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani.

Social Plugin