Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KIKWETE AWASILI MKOANI TABORA KWA ZIARA YA KIKAZI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewasili mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi inayolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuzindua miradi mbalimbali pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi ili kutafuta ufumbuzi wake.

Mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kikwete amesaini kitabu cha wageni ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi ziara hiyo ambayo inatarajiwa kugusa sekta mbalimbali za maendeleo katika mkoa huo.

Katika ziara yake, Waziri huyo atatembelea miradi inayotekelezwa chini ya Serikali, kukagua maendeleo yake, kujionea hatua zilizofikiwa pamoja na kutoa maelekezo ya kuboresha utekelezaji wake ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye tija.

Aidha, ziara hiyo itatoa fursa kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora kuwasilisha maoni, changamoto na mapendekezo yao moja kwa moja kwa Serikali, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hatua hiyo ni kutokana na Serikali kusisitiza umuhimu wa viongozi kuwafikia wananchi kupitia ziara za kikazi, hatua inayochangia kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya Watanzania.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com