Baadhi ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wamewataka vijana kuepuka kushiriki kwenye maandamano yanayoweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi, wakisema mazingira ya amani ndiyo msingi wa maisha ya kila siku, shughuli za kiuchumi na maendeleo ya wananchi.
Akizungumza na chombo hiki cha habari leo Jumamosi Julai 04, 2026, Mkazi wa Magomeni Jijini Dar es Salaam, Bibi Neema Mkasi amesema vijana wanapaswa kuepuka kufuata mikumbo inayoweza kuwaingiza katika matatizo, akieleza kuwa watu wengi wenye kipato cha chini hawana akiba ya chakula wala fedha za kuwasaidia endapo kutatokea vurugu.
"Mama Samia awe na amani, vijana tuwatake wasifuate mikumbo, wataumia na kuathirika, waache, wajipe muda wa kushughulika. Wengi tunaishi maisha ya chini, hatuna akiba yoyote ya chakula wala fedha, kwa hiyo vurugu zikitokea sisi wa hali ya chini kiuchumi ndio tutaathirika zaidi." amesema Bi. Mkasi.
Kwa upande wake Bw. Madandi Donald, mjasiriamali wa Ilala Dar Es Salaam amesema kuwa amani ni nguzo muhimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali, akibainisha kuwa mazingira ya utulivu ndiyo yanayowezesha wananchi kujipatia kipato na kuendesha shughuli zao bila hofu, akisema wananchi wengi wanategemea shughuli za kila siku kujikimu, hivyo machafuko yanaweza kusababisha hasara kubwa kwa wananchi wa kawaida.
Aidha katika hatua nyingine wananchi hao wamehimiza kila Mtanzania kuendelea kulinda amani, utulivu na mshikamano wa taifa, wakisisitiza kuwa maendeleo ya nchi yanategemea mazingira salama yanayowapa wananchi fursa ya kufanya kazi, kuendesha biashara na kujenga uchumi wao bila hofu ya machafuko.


Social Plugin