Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma kupitia kwa Kamanda wa Mkoa huo Philimon Makungu, limesema uchunguzi wa kisayansi kuhusu kifo cha mwanachama wa CHADEMA na aliyekuwa Dereva wa John Heche, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Suezi Dani Maradufu, unaendelea huku sampuli mbalimbali zikichukuliwa kwaajili ya uchunguzi zaidi ili kuthibitisha chanzo halisi cha kifo chake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma leo Ijumaa Julai 3, 2026, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kisayansi na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Bugando pamoja na wataalamu kutoka mikoa ya Geita na Dodoma, wakishirikiana na Afisa Mwandamizi kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Uchunguzi huo umefanyika mbele ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na ndugu wa marehemu.
Polisi wamesema baada ya uchunguzi huo, sampuli zimechukuliwa kwaajili ya uchunguzi wa kina zaidi wa kisayansi ili kuthibitisha chanzo halisi cha kifo, na kwamba matokeo yatakapokamilika yataisaidia mamlaka husika kubaini kilichosababisha kifo hicho.
Maradufu alifariki Julai 1, 2026 ndani ya chumba alichokuwa amepanga katika nyumba ya kulala wageni ya Ntahamba mkoani Kigoma. Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa, huku CHADEMA ikitaka kufanyika kwa uchunguzi huru na wa kina ili kubaini mazingira ya kifo chake.
Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa uchunguzi unaendelea kwa kufuata taratibu za kisayansi na kisheria, na limewataka wananchi kuwa na subira wakati wataalamu wakikamilisha uchunguzi huo.



Social Plugin