Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Lucy Mayenga, akizungumza wakati akizindua ugawaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo zaidi ya Milioni 86 uliofanyika katika Shule ya Sekondari Igaga Julai 18, 2026
Na Sumai Salum- Kishapu
Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Lucy Mayenga, amesema Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa sekta muhimu za huduma za jamii.
Mhe. Mayenga ameyasema hayo Julai 18, 2026 wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo uliofanyika katika Shule ya Sekondari Igaga, ambapo vifaa mbalimbali pamoja na fedha vilikabidhiwa kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa miradi katika kata mbalimbali za Jimbo la Kishapu.
Amesema jumla ya shilingi milioni 86,228,000 zimetengwa kupitia Mfuko wa Jimbo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, fedha ambazo zitatekeleza jumla ya miradi 30 ndani ya Kata 26 kati ya 29, ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukamilishaji wa zahanati,Shule za msingi na Sekondari, kituo cha Polisi Maganzo, Kituo cha Afya pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Dkt. Jakaya Kikwete.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa fedha za Serikali zinapaswa kutumika kwa uadilifu na uwajibikaji ili ziweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi. Pia amegusia changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa baadhi ya wakandarasi wa miradi ya maji, akiahidi kuendelea kuzifuatilia na kuzizungumza katika mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali huku akieleza kuwa maendeleo ni hatua na yataendelea kupatikana kupitia usimamizi mzuri wa miradi. Pia aliwahamasisha wanawake kujiunga na majukwaa ya wanawake ya kujikwamua kiuchumi ili kuongeza kipato na kujiletea maendeleo. Aliongeza kuwa katika kipindi cha Awamu ya Sita, miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa Kishapu na maeneo mengine nchini kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Lucy Mayenga akiendelea kuzungumza
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mhe. Josephat Limbe, amesema Halmashauri imepokea zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Alibainisha kuwa kata 26 kati ya 29 zimepokea fedha kutoka Mfuko wa Jimbo baada ya miradi yake kuridhiwa na Ofisi ya Mipango ya Halmashauri.
Naye Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Maziku Guna kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, amesema fedha hizo za Mfuko wa Jimbo zimegusa takribani vijiji 30 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Diwani wa Kata ya Igaga, Mhe. James Kija, amemshukuru Mbunge kwa kuichagua Igaga kuwa mwenyeji wa uzinduzi huo. Ameeleza kuwa pamoja na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa, bado Kata ya Igaga inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari Igaga.
Aidha, ameomba mradi wa maji wa zaidi ya shilingi milioni 500 unaotekelezwa katika Kata ya Igaga uendelee kupewa kipaumbele ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa kiwango kinachohitajika.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Igaga "B", Sophia James, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo na kueleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi wa Kishapu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Josephat Limbe akizungumza wakati uzinduzi wa ugawaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo zaidi ya Tsh. Milioni 86 uliofanywa na Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Lucy Mayenga katika Shule ya Sekondari Igaga Julai 18, 2026
Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Maziku Gunah akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Emmanuel Johnson, wakati uzinduzi wa ugawaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo zaidi ya Tsh. Milioni 86 uliofanywa na Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Lucy Mayenga katika Shule ya Sekondari Igaga Julai 18, 2026
Diwani wa Kata ya Igaga, Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. James Kija akizungumza wakati uzinduzi wa ugawaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo zaidi ya Tsh. Milioni 86 uliofanywa na Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Lucy Mayenga katika Shule ya Sekondari Igaga Julai 18, 2026
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Igaga "B" Kata ya Igaga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Sophia James
Social Plugin