
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, amesema kuwa maridhiano ni msingi mkuu wa kuponya taifa, kurejesha umoja wa wananchi na kujenga uongozi wenye mamlaka ya kimaadili.
Akitoa mtazamo wake kupitia mitandao ya kijamii, alieleza kuwa uzoefu wake katika kufundisha somo la Falsafa ya Siasa chuoni, pamoja na uchambuzi wa nyaraka za maridhiano kutoka nchi mbalimbali duniani kama vile Afrika Kusini, Rwanda, Kenya, Sierra Leone, Gambia na Cyprus, unathibitisha kuwa maridhiano hayawezi kuepukika pale ambapo taifa linapokuwa limegawanyika kutokana na matukio ya kihalifu au migogoro mikubwa.
Alifafanua kuwa maridhiano ya dhati hutoa fursa muhimu ya kukiri makosa na kuruhusu jamii kuanza upya, kujifunza kuwajibika kwa jamii hata kwa wale wanaoamini wameshinda, na kuzuia historia ya migogoro isije ikatumika baadaye kama silaha ya kisiasa.
Aidha, alisisitiza kuwa mchakato huo unarejesha mamlaka ya kimaadili kwa viongozi kupitia kujenga uongozi unaotokana na ushawishi badala ya kutumia nguvu, huku akionya kuwa hakuna kundi lenye ushawishi ambalo linapaswa kuachwa nje ya mchakato huo ili kuepusha hatari ya kuvuruga utekelezaji wa makubaliano.
Akizungumzia faida za mazungumzo ya wazi, Askofu Bagonza alisema kuwa mafanikio makubwa ya maridhiano ni kuondoa hisia za kisasi na kujenga upya imani iliyopotea kati ya wananchi na viongozi wao.
Alionya kuwa jamii inayokataa kuzungumza inaendelea kubeba majeraha ya ndani ambayo huhatarisha usalama na kujitokeza tena kila kunapotokea tofauti za kijamii au kisiasa, na ndio maana maridhiano hayo lazima yajengwe juu ya nguzo thabiti za ukweli, uwajibikaji na msamaha ili yawe na tija ya kudumu.
Askofu Bagonza alisisitiza kuwa pale wananchi wanaporejesha imani yao kwa viongozi na taasisi za nchi, taifa hufurahia utulivu, mshikamano mkubwa na kupata mazingira mazuri ya kuleta maendeleo endelevu.
Alieleza kuwa hatua hiyo si tu suluhu ya sasa, bali ni uwekezaji wa kimkakati na wa maana sana kwa ajili ya usalama na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Social Plugin