Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HALI NI SHWARI MPAKA WA TUNDUMA, WANANCHI WAENDELEA NA SHUGHULI ZAO KAMA KAWAIDA




Na Mwandishi Wetu ,Songwe

Hali ya utulivu na amani imeendelea kutawala katika eneo la Mpakani Tunduma, mkoani Songwe, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku bila changamoto yoyote ya kiusalama.

Katika ziara iliyofanyika leo eneo la mpaka huo, shughuli mbalimbali za kiuchumi ziliendelea kama kawaida, zikiwemo biashara ndogondogo, usafirishaji wa mizigo, huduma za fedha, pamoja na harakati za wasafiri wanaovuka mpaka kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Madereva wa malori ya mizigo waliendelea na safari zao, wafanyabiashara walifungua maduka yao kama ilivyo kawaida, huku wananchi wengine wakionekana wakifanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato katika maeneo ya mpakani.

Pia, vyombo vya ulinzi na usalama vimeendelea kutekeleza majukumu yake ya kawaida ya kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unaimarishwa, hali iliyochangia kuendelea kuwepo kwa mazingira tulivu yanayowezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika bila usumbufu.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na CENTRAL walisema wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa utulivu, wakisisitiza umuhimu wa kulinda amani ambayo imekuwa msingi wa biashara na maendeleo katika eneo hilo muhimu la kimkakati.

Mpaka wa Tunduma ni miongoni mwa mipaka mikubwa inayounganisha Tanzania na nchi jirani, ukiwa na mchango mkubwa katika biashara ya kikanda na usafirishaji wa bidhaa ndani ya ukanda wa Kusini mwa Afrika. Kuendelea kuwepo kwa utulivu katika eneo hilo kunachochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya mataifa jirani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com