Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIRA YA TAIFA 2050 YAIPA SEKTA YA MADINI MWELEKEO MPYA WA KUCHOCHEA UCHUMI.

Mwenyekiti wa Tume ya madini Dkt.Janet R.Lekashingo akiwa katika banda la tume ya madini ya Maonesho ya sabasaba wa wapili kutoka kushoto akikagua madini yaliyowekwa katika banda hilo la Tume ya madini 
Mwenyekiti wa Tume ya madini Dkt.Janet R.Lekashingo wa kwanza kulia akioneshwa bidhaa zilizowekwa katika banda la maonesho ya sabasaba wakati alipotembelea taasisi zilizopo chini ya Wizara ya madini

Na Mwandishi wetu Malunde 1-Blog  Dar es Salaam.

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeipa sekta ya madini jukumu la kimkakati la kuongoza mageuzi ya uchumi wa Tanzania kupitia uongezaji thamani wa madini, matumizi ya teknolojia za kisasa na ushirikishwaji wa watanzania katika shughuli za uchimbaji. 

Mwenyekiti wa Tume ya madini, Dkt. Janet R. Lekashingo, amesema Tume imejipanga kutekeleza malengo ya dira hiyo ili sekta ya madini iwe nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu nchini.

Akizungumza  baada ya kutembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya madini katika Kijiji cha madini kwenye Maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Dkt. Lekashingo amesema utekelezaji wa Dira ya 2050 utazingatia kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi, kuimarisha utafiti wa jiolojia kubaini maeneo mapya yenye rasilimali za madini, pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na zinazoongeza usalama migodini.

Aidha, amewahimiza wananchi kutembelea banda la Tume ya madini ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa madini, ikiwemo taratibu za kushiriki biashara ya madini na kuuza madini kupitia masoko na vituo rasmi vya ununuzi. 

Pia amewapongeza viongozi na watumishi wa Tume kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku akiwataka kuongeza juhudi ili kufikia lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.4 katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Katika ziara hiyo, Dkt. Lekashingo ametembelea mabanda ya taasisi mbalimbali za Wizara ya madini, ikiwemo STAMICO, GST na TGC, kabla ya kutembelea mabanda ya JKCI, Zanzibar na Wizara ya Nishati. 

Akiwa katika banda la Wizara ya Nishati, ameiomba TANESCO kuhakikisha umeme unafikishwa katika maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ili kuongeza tija kwa wachimbaji, kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya madini na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com