Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050 YAIPA SEKTA YA MADINI MWELEKEO MPYA WA KUCHOCHEA UCHUMI

📍Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet  Lekashingo, amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeipa sekta ya madini nafasi ya kimkakati ya kuongoza mageuzi ya uchumi wa Tanzania kupitia uongezaji thamani wa madini, ushirikishwaji wa watanzania na matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za uchimbaji wa madini.

Akizungumza mapema leo Julai 6, 2026, alipotembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini katika Kijiji cha Madini kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Dkt. Lekashingo amesema Tume ya Madini imejipanga kikamilifu kutekeleza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ili sekta ya madini iwe nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.

Amesema utekelezaji wa dira hiyo unalenga kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi badala ya kuyasafirisha ghafi, kuimarisha utafiti wa jiolojia ili kubaini maeneo mapya yenye rasilimali za madini, kuongeza ushiriki wa watanzania katika miradi ya uchimbaji wa madini pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na zinazoongeza usalama migodini.

Aidha, amewataka wananchi kutembelea banda la Tume ya Madini ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Tume pamoja na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa madini, ikiwemo taratibu za kushiriki biashara ya madini na kuuza madini kupitia masoko na vituo vya ununuzi wa madini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Lekashingo amewapongeza viongozi na watumishi wa Tume ya Madini kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2025/2026, akisema mafanikio hayo yanadhihirisha uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa sekta ya madini.

“Mmetuheshimisha kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato, lakini tusibweteke. Bado tuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha tunavuka lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.4 katika mwaka wa fedha 2026/2027,” amesema.

Wakati huohuo, Dkt. Lekashingo ametembelea mabanda mbalimbali ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini, ikiwemo Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na Wadau wa Madini kabla ya kutembelea mabanda ya Taasisi ya Moyo  ya Jakaya Kikwete (JKCI), Banda la Zanzibar na Wizara ya Nishati.

Akiwa katika banda la Wizara ya Nishati, Dkt. Lekashingo ameiomba Wizara hiyo kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha umeme unafikishwa katika maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini nchini ili kuongeza tija kwa wachimbaji, kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya madini na kuendeleza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com