>Asema kasi ya maendeleo chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amani, uchumi, afya, maji na miundombinu vimemshawishi kubadili msimamo wa kisiasa.
Na Oscar Assenga,TANGA
Baada ya zaidi ya miaka 30 ya kuwa mwanasiasa wa upinzani, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe, amefanya uamuzi mkubwa wa kisiasa kwa kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jumbe, ambaye kwa muda mrefu alikuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa Chadema mkoani Tanga, amesema uamuzi wake umetokana na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na juhudi za Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha amani, umoja na ustawi wa wananchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumpokea ndani ya CCM iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurhaman leo,Jumbe alisema hakufanya uamuzi huo kwa papara, bali baada ya kutafakari kwa kina na kujiridhisha kuhusu mwelekeo wa maendeleo ya Taifa.
"Nilikuwa mpinzani kwa zaidi ya miaka 30, lakini leo nimeamua kuhitimisha safari hiyo. Kilichonishawishi zaidi ni kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea Watanzania maendeleo na kuhakikisha amani ya nchi inalindwa," alisema.
Alieleza kuwa pia amevutiwa na utekelezaji wa falsafa ya 4R inayosisitiza maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya, akisema imeongeza mshikamano na kuimarisha mazingira ya maendeleo nchini.
Akizungumzia Mkoa wa Tanga, Jumbe alisema mabadiliko yanayoonekana katika sekta mbalimbali ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya kuufungua mkoa huo kiuchumi.
Alitaja kuongezeka kwa shughuli katika Bandari ya Tanga, ujenzi wa bandari kavu pamoja na utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati kuwa miongoni mwa hatua zilizochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za biashara.
"Nimekuwa nikipaza sauti kwa miaka mingi nikitaka Tanga ifunguliwe kiuchumi. Leo naona hilo limefanyika. Mizigo imeongezeka bandarini, bandari kavu zimejengwa na shughuli za biashara zinaendelea kukua," alisema.
Katika sekta ya afya, Jumbe alisema maboresho yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na ujenzi wa zahanati katika kata na mitaa mbalimbali vimempa imani kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma kwa wananchi.
Aidha, alisema upanuzi wa huduma za maji na umeme pamoja na utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni miongoni mwa hatua zinazoonyesha dhamira ya Serikali ya kuinua maisha ya Watanzania.
"Nilijiuliza ni hoja gani itanifanya nibaki upinzani wakati maendeleo yanaonekana wazi. Tanga ina amani, huduma zinaimarika na wananchi wanaendelea kunufaika na miradi ya maendeleo," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurhaman, alisema chama hicho kinaendelea kuimarisha umoja na mshikamano ili kuongeza uwezo wake wa kusimamia maendeleo na kuwatumikia wananchi.
Alisema tangu alipopewa dhamana ya kuongoza CCM mkoani humo, ameweka mkakati wa kuimarisha chama kupitia ushirikiano na wanachama pamoja na kuwakaribisha viongozi kutoka vyama vingine vya siasa.
Rajab alisema mkakati huo umeendelea kuzaa matunda, akieleza kuwa kujiunga kwa Rashid Jumbe ni ishara ya kuongezeka kwa imani ya baadhi ya viongozi wa upinzani kwa juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali.
"Jumbe alikuwa mmoja wa viongozi wakubwa wa upinzani katika Wilaya ya Tanga. Tuliahidi kwamba tutamshawishi aje kushirikiana nasi katika kujenga chama na kuwaletea wananchi maendeleo, na leo tumefanikiwa," alisema.
Social Plugin