Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TOSCI YAENDELEA NA MSAKO WA WAUZAJI WA MBEGU FEKI KULINDA MASLAHI YA WAKULIMA



Na Wellu Mtaki, Dodoma.

Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imeendelea kuimarisha msako dhidi ya watu wanaojihusisha
na uuzaji wa mbegu feki kwa wakulima nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda uzalishaji wa mazao na kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora zenye tija.

Kauli hiyo imetolewa na Mtafiti na Mkaguzi wa Mbegu kutoka TOSCI Makao Makuu, Neema Yohana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kufanyika jijini humo.

Amesema kuwa hapo awali tatizo la uuzaji wa mbegu feki lilikuwa kubwa na liliwasababishia wakulima hasara kutokana na mavuno duni, lakini kwa sasa hali imeimarika kwa kiasi kikubwa kufuatia matumizi ya nembo maalum za ubora zinazotolewa na TOSCI.

“Changamoto ya mbegu feki ilikuwepo kwa kiwango kikubwa miaka ya nyuma, lakini tangu tuanze kutumia nembo za ubora, tatizo hilo limepungua sana. Tunaendelea kuimarisha ukaguzi na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaojihusisha na kughushi au kuuza mbegu feki kwa wakulima,” amesema Neema.

Amefafanua kuwa TOSCI inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya pembejeo za kilimo nchini kote ili kubaini na kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kuwaathiri wakulima.

Kwa mujibu wake, mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yanaonyesha kuwa hatua zinazochukuliwa na taasisi hiyo zimezaa matunda, kwani visa vya mbegu feki vimepungua kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na miaka iliyopita.

Aidha, amesema ushiriki wa TOSCI katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma unalenga kutoa elimu kwa wakulima, wafanyabiashara wa mbegu pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora na namna ya kuzitambua.

“Tunatoa huduma mbalimbali kwa wakulima na wafanyabiashara wa mbegu. Tumeona bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu, hivyo tunatumia fursa hii kuwaelimisha wananchi namna ya kutambua mbegu bora na zisizo bora ili waweze kufanya maamuzi sahihi wanaponunua mbegu,” amesema.

Sambamba na hilo, amewahimiza wakulima na wananchi kuhakikisha wanajiridhisha kuhusu uhalali wa mbegu wanazonunua kwa kutumia mfumo wa uhakiki wa TOSCI uliowekwa kwenye lebo za ubora.

Amesema kuwa mnunuzi anatakiwa kukwangua sehemu maalum ya lebo ya TOSCI iliyopo kwenye kifurushi cha mbegu kisha kufuata maelekezo kwa kupiga namba *148*52#, ambapo atapata taarifa zinazothibitisha kama mbegu hiyo ni halali au la.

“Mbegu bora zilizothibitishwa na TOSCI zina lebo maalum za ubora. Mkulima anapaswa kukwangua lebo hiyo na kufuata maelekezo kupitia namba 14852#. Mwisho wa zoezi hilo atapata ujumbe kwenye simu yake utakaoonyesha uhalali wa mbegu husika. Akipata taarifa zisizo sahihi, basi ajue mbegu hiyo inaweza kuwa feki,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya mbegu feki utasaidia serikali na wadau wa sekta ya kilimo kuendelea kulinda maslahi ya wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com