NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) imewahimiza wananchi na wadau wa maendeleo kutembelea banda lake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kupata huduma mbalimbali na elimu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake.
Wito huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Wizara katika maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, jijini Dar es Salaam, kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026.
OWM-TAMISEMI imesema ushiriki wake katika maonesho hayo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kuimarisha uwazi na uwajibikaji, pamoja na kutoa elimu kuhusu huduma na majukumu yanayotekelezwa na Wizara na taasisi zake.
Aidha, wananchi watakaotembelea banda la TAMISEMI watapata fursa ya kufahamu kwa undani utekelezaji wa bajeti ya Serikali, usimamizi wa rasilimali za Taifa, pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia Wizara na taasisi zilizo chini yake.
Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) mwaka huu yanabebwa na kaulimbiu isemayo, "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania," huku yakienda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo.
Kupitia ushiriki huo, OWM-TAMISEMI inalenga kuendelea kuimarisha mawasiliano na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali za Mitaa, pamoja na kuwapa wadau nafasi ya kutoa maoni na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na utoaji wa huduma kwa umma.




Social Plugin