Na Beda Msimbe, TBN, Moscow - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo jijini Moscow kwa ajili ya ziara ya kitaifa nchini Urusi inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi na kihistoria kati ya Tanzania na Urusi.
Ziara hii ni ya kihistoria kwani ni mara ya pili kwa Rais wa Tanzania kufanya ziara ya aina hiyo nchini Urusi tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa nchi hizo. Ziara ya kwanza ilifanywa miaka ya 1960 na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Kupitia ziara hiyo, Rais Samia anaendelea kutekeleza mkakati wa kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na mataifa mbalimbali duniani ili nchi iweze kunufaika zaidi kiuchumi kupitia uwekezaji, biashara na maendeleo ya rasilimali watu.
Akiwa nchini Urusi, Rais Samia anatarajiwa kushiriki katika mkutano mkubwa wa uwekezaji utakaofanyika jijini St. Petersburg, ambapo ataitangaza Tanzania kama kitovu cha uwekezaji na fursa za biashara. Aidha, atafanya mazungumzo yanayolenga kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali, ikiwemo maendeleo ya rasilimali watu, jambo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Rais Samia aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Vnukovo majira ya saa 2:25 usiku kwa saa za Moscow, ambapo alipokelewa kwa heshima ya kupigiwa wimbo wa taifa na kukaguliwa kwa gwaride rasmi.
Katika mapokezi hayo, Rais Samia alipokewa na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Shirikisho la Urusi, Maxim Reshetnikov, pamoja na viongozi wengine wa serikali ya Urusi.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, leo Rais Samia ataweka shada la maua katika Kaburi la Askari Asiyejulikana kabla ya kuelekea Ikulu ya Kremlin kwa mazungumzo rasmi na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.



Social Plugin