
Mkurugenzi wa Shirika la Water for Good Devocatus Kamala akisalimiana na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni wakati wa hafla ya kukabidhi matundu 15 ya vyoo yaliyojengwa na shirika hilo shule ya msingi Masekelo

Shirika la Water for Good limejenga matundu 15 ya vyoo vya kisasa katika Shule ya Msingi Masekelo iliyopo Kata ya Bukene, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, hatua iliyowezesha zaidi ya wanafunzi 400 kuondokana na changamoto ya ukosefu wa vyoo salama na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo leo Juni 2, 2026, Mkurugenzi wa Shirika la Water for Good, Devocatus Kamala, amesema ujenzi wa vyoo hivyo ulifanyika baada ya kubainika kuwa shule hiyo ilikuwa na miundombinu ambayo imechakaa ambayo ilikuwa ikisababisha usumbufu mkubwa.
Amesema kabla ya utekelezaji wa mradi huo, baadhi ya wanafunzi walilazimika kurudi nyumbani kwenda kujisaidia huku wengine wakisubiri kwa muda mrefu kupata nafasi ya kutumia vyoo vilivyokuwepo, hali iliyokuwa ikiathiri muda wao wa masomo.
“Tumehakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia na changamoto ya vyoo katika shule hii imekwisha tumejenga matundu 15 ya vyoo vya kisasa,” amesema Kamala.
Mbali na mradi huo, Kamala amesema shirika hilo pia limejenga zahanati Kijiji cha Sumbigu ili kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi, ambapo miradi hiyo miwili imegharimu zaidi ya shilingi milioni 56.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, amesema ujenzi wa vyoo hivyo utachangia kuongeza kiwango cha ufaulu na kuondoa tatizo la miundombinu ya vyoo.
Amewashukuru wadau wa maendeleo, hususan Shirika la Water for Good, kwa mchango wao katika kuboresha sekta za elimu na afya na kusaidia jamii kupata huduma muhimu karibu na maeneo yao.







Social Plugin