Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

EAC YATAKA SHERIA IMARA KULINDA WATUMIAJI WA MITANDAO YA KIJAMII


Na Bora Fadhili, Arusha.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imezitaka serikali za nchi wanachama kuharakisha uundaji na uimarishaji wa sheria pamoja na sera madhubuti zitakazolinda watumiaji wa mitandao ya kijamii dhidi ya unyanyasaji wa kidijitali, huku wanawake na watoto wa kike wakitajwa kuwa miongoni mwa waathirika wakubwa wa matumizi mabaya ya teknolojia.

Akizungumza Juni 26,2026 katika Kilele cha Kongamano la Pili la Mazungumzo ya Kizazi kwa Kizazi la Wanawake wa EAC, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake la Jumuiya hiyo, Fatuma Ndangiza, amesema matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamechangia kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia.

 Amesema hali hiyo inahitaji hatua za haraka kutoka kwa serikali na mabunge ya nchi wanachama ili kuimarisha mifumo ya kisheria itakayowalinda watumiaji wa majukwaa ya kidijitali.

Pia amesema ni muhimu kuongeza uwekezaji katika elimu ya usalama wa kidijitali, hasa kwa wanawake na wasichana, ili kuwajengea uwezo wa kutambua, kujikinga na kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanyika mtandaoni. Ameeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria, elimu na uelewa wa matumizi salama ya teknolojia ni msingi muhimu wa kujenga mazingira salama ya kidijitali kwa wananchi wote.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dkt. Gladness Salema, amesema vijana wanapaswa kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kuzingatia maadili katika matumizi ya teknolojia. 

Amesema majukwaa ya kidijitali yanapaswa kutumika kujifunza, kukuza ubunifu, kuanzisha biashara, kutafuta ajira pamoja na kushiriki katika maendeleo ya jamii, badala ya kusambaza taarifa potofu, lugha za chuki na vitendo vinavyochochea migogoro.

Amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya teknolojia yatachangia kujenga jamii salama, yenye maadili na inayotumia fursa za kidijitali kwa maendeleo ya wananchi na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com