📍 Je, nyuma ya hofu dhidi yake kuna ukweli au ni imani zilizojengeka kwa muda mrefu?
Na Beatus Maganja
Fikiria maisha ya kuishi ukihukumiwa kwa kosa ambalo hulijui na hukuwahi kulitenda. Kila unapojitokeza, watu wanakukimbia. Kila sauti yako inaposikika, mioyo ya watu inajaa hofu. Kila unapoonekana sehemu, wengine huanza kuhesababu mikosi ambayo hata haijatokea. Sasa hayo ndiyo maisha ya bundi.
Bundi alikosea nini?Je, kosa lake ni kufanya shughuli zake usiku? Je, kosa lake ni kuwa na macho makubwa yanayong'aa gizani? Je, kosa lake ni kutoa sauti ambazo wengi wetu hatujazizoea? Au kuna jambo lingine ambalo limemfanya ndege huyu kuwa mmoja wa viumbe wanaoogopwa zaidi katika jamii nyingi za kiafrika hususan Tanzania?
Kwa karne nyingi, bundi amekuwa akiishi katika kivuli cha hofu za binadamu. Katika baadhi ya maeneo, kuonekana kwake au kusikika kwa sauti yake usiku kumekuwa kukihusishwa na mikosi, vifo au matukio mabaya yanayotarajiwa kutokea. Mara nyingi watu humwona na kuingiwa na hofu kabla hata hawajajua yeye ni ndege wa aina gani.
Lakini swali kubwa ni hili, je, bundi ndiye anayesababisha matukio hayo, au ni tafsiri ambazo binadamu tumekuwa tukizipa tabia zake kwa muda mrefu?
Ukweli ni kwamba bundi ni mmoja wa ndege wenye uwezo mkubwa wa kuwinda usiku. Wakati viumbe wengine wanapokuwa wamelala, yeye huamka na kuanza kazi yake ya kutafuta chakula.
Macho yake makubwa, masikio yake yenye uwezo wa kusikia kwa umakini mkubwa na uwezo wake wa kuruka kimya kimya humfanya kuwa mwindaji mahiri wa panya, wadudu na viumbe wengine wadogo.
Kwa maneno mengine, wakati wengine wanamwogopa, bundi huwa anafanya kazi muhimu ya kusaidia kudhibiti viumbe wanaoweza kuharibu mazao au kusababisha usumbufu kwa binadamu.
Hebu fikiria kwa muda.
Mkulima anayelala usiku akiwa hajui kuwa kwenye shamba lake kuna panya wanaotafuna mazao. Wakati huo huo, bundi yuko kazini. Bila mshahara. Bila kupewa tuzo yoyote.
Akipunguza idadi ya panya ambao wangetumia miezi mingi kuharibu jasho la mkulima. Lakini badala ya kupongezwa, mara nyingi amekuwa akifukuzwa, kupigwa mawe au hata kuuawa kutokana na imani mbalimbali zilizojengeka katika jamii.
Lakini vipi kuhusu bundi anayelia karibu na nyumba za watu? Je, hiyo ni ishara ya msiba? Hadi leo hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa sauti ya bundi husababisha au kutabiri kifo cha binadamu. Mara nyingi hutoa sauti kwa ajili ya mawasiliano, kutangaza himaya yake, kutafuta mwenza au kuwasiliana na watoto wake.
Msiba unapotokea baada ya sauti hiyo, binadamu huikumbuka na kuihusisha nayo, lakini husahau mara nyingi ambazo bundi alilia na hakuna jambo lolote baya lililotokea.
Jambo la kushangaza ni kwamba katika sehemu nyingine duniani, bundi huchukuliwa kuwa alama ya hekima, maarifa na akili.Mfano, Ugiriki ya kale, bundi aliheshimiwa kama alama ya hekima na maarifa na katika maeneo kadhaa ya Japan akionekana kuwa ishara ya bahati njema na ulinzi.
Hivyo, wakati jamii moja ikimwona kama ishara ya mkosi, jamii nyingine humwona kama ishara ya busara. Nani yuko sahihi? Je ni mitazamo yetu au tamadunI zetu?!!
Labda jibu si kuhusu bundi. Labda jibu lipo katika namna sisi binadamu tunavyotafsiri vitu tusivyovielewa kikamilifu.Kadiri sayansi inavyoendelea kutufundisha kuhusu maumbile na tabia za wanyamapori, ndivyo tunavyozidi kugundua kuwa viumbe wengi tunaowaogopa hawana uadui wowote dhidi yetu. Mara nyingi wao wanakuwa wakifanya kazi zao za kawaida za kuishi kama walivyoumbwa kufanya.
Pengine wakati umefika wa kumuona bundi kwa mtazamo mpya. Si kama mjumbe wa mikosi.Si kama ishara ya hofu.Bali kama mmoja wa viumbe wa ajabu ambao Mungu amejaalia kuishi katika sayari hii, akiwa na nafasi yake muhimu katika mfumo wa ikolojia. Kwa sababu mwisho wa siku, swali bado linabaki pale pale.Bundi alikosea nini hadi kuogopwa hivi?
Kwa "Take-Take" kama hizi, endelea kubaki katika kurasa za TAWA+255 676 475 541#TumerithishwaTuwarithishe

Social Plugin