Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MRADI WA ReSea WAKABIDHI VIFAA VYA UZALISHAJI KUIMARISHA UCHUMI WA BULUU NA MAISHA ENDELEVU PEMBA


Na Mwandishi Wetu, Pemba

Jamii za Pwani kisiwani Pemba zinatarajiwa kunufaika zaidi na fursa za uchumi wa buluu baada ya Mradi wa Regenerative Seascapes for People, Climate and Nature (ReSea) kukabidhi vifaa vya uzalishaji kwa vikundi vya Biashara za Uchumi wa Buluu (Blue Economy Enterprises – BEE) vinavyoongozwa na wanawake, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, kipato na ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Makabidhiano hayo yamefanyika  wakati wa ziara rasmi ya Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, aliyeshiriki hafla hiyo pamoja na viongozi wa Mradi wa ReSea, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Women Fund Tanzania Trust (WFTT), Rose Marandu, Mkurugenzi wa Mradi wa ReSea kutoka Mission Inclusion, Andreanne Martel, pamoja na Mwakilishi wa IUCN Tanzania, Charles Oluchina.

Katika hafla hiyo, vikundi mbalimbali vya wanawake vimekabidhiwa vifaa vitakavyowawezesha kuendeleza shughuli za uchumi wa buluu, ikiwemo kilimo na uchakataji wa mwani, ufugaji wa matango bahari (sea cucumber), unenepeshaji wa kaa pamoja na uchakataji wa dagaa. 

Vifaa hivyo vinatarajiwa kuongeza tija ya uzalishaji, kuinua kipato cha wanufaika na kuimarisha maisha endelevu ya jamii zinazotegemea rasilimali za bahari.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Women Fund Tanzania Trust (WFTT), Rose Marandu, amesema uwezeshaji wa wanawake na vijana ni sehemu muhimu ya mafanikio ya uchumi wa buluu na maendeleo endelevu ya jamii.

"Makabidhiano haya yanaonyesha dhamira yetu ya kuhakikisha wanawake na vijana wanapata zana na uwezo wa kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu kwa njia endelevu. Tunataka kuona wanakuwa na kipato bora huku wakishiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira ya bahari na pwani," amesema Marandu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa ReSea kutoka Mission Inclusion, Andreanne Martel, amesema mafanikio ya mradi yanatokana na ushirikiano imara kati ya jamii, serikali na washirika wa maendeleo.

"ReSea inaamini kuwa jamii ndiyo msingi wa mafanikio ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya uchumi wa buluu. Kupitia ushirikiano huu tunaendelea kujenga uwezo wa wananchi kutumia rasilimali za bahari kwa njia endelevu huku tukiongeza ustahimilivu wao dhidi ya mabadiliko ya tabianchi," amesema Martel.

Naye Mwakilishi wa IUCN Tanzania, Charles Oluchina, amesema mradi huo unaonyesha namna uhifadhi wa mazingira unavyoweza kwenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi ya wananchi.

"Tunataka kuona jamii zinakuwa walinzi wa mazingira huku zikinufaika moja kwa moja na rasilimali za bahari. Suluhisho zinazotegemea asili zina mchango mkubwa katika kulinda mifumo ya ikolojia na kujenga uchumi imara kwa vizazi vya sasa na vijavyo," amesema Oluchina.

Mbali na makabidhiano ya vifaa, viongozi hao wamezindua rasmi Kituo cha Kujifunzia cha Jamii cha Chamanangwe, kitakachotumika kama kitovu cha kujenga uwezo wa jamii, kubadilishana uzoefu na maarifa pamoja na kuendeleza matumizi ya Suluhisho Zinazotegemea Asili (Nature-based Solutions – NbS) katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia kituo hicho, jamii pamoja na viongozi wa maeneo husika watapata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za kuhifadhi mifumo ya ikolojia ya bahari na pwani, kuendeleza shughuli endelevu za uchumi wa buluu na kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Makabidhiano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa nguzo ya Blue People Pillar ya Mradi wa ReSea inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na jamii za pwani kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi wa buluu kwa njia endelevu, huku ikichochea uhifadhi wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali za bahari.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa ReSea umetembelea pia vikundi vinavyonufaika na mradi huo ili kujionea mafanikio ya shughuli zinazotekelezwa katika jamii. 

Miongoni mwa vikundi vilivyotembelewa ni Kikundi cha Almujitahid cha Wilaya ya Chake Chake kinachojishughulisha na unenepeshaji wa kaa, uongezaji thamani wa mwani pamoja na urejeshaji wa mikoko.
Ujumbe huo pia umetembelea Kikundi cha Tusijisahau kilichopo Wilaya ya Mkoani, ambacho kinatekeleza shughuli za mnyororo wa thamani wa mwani pamoja na kusimamia eneo la maonesho ya Suluhisho Zinazotegemea Asili kwa ajili ya urejeshaji wa mfumo wa ikolojia wa mikoko.

Viongozi wa mradi wamesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali ya Canada, taasisi zinazotekeleza mradi, serikali na jamii za pwani unaendelea kuwa msingi muhimu wa kujenga uchumi wa buluu unaozingatia uhifadhi wa mazingira, urejeshaji wa mifumo ya ikolojia na ustawi wa wananchi.

Mradi wa Regenerative Seascapes for People, Climate and Nature (ReSea) unatekelezwa katika Tanzania, Kenya, Msumbiji, Madagascar na Comoro ukiwa na lengo la kuimarisha usimamizi shirikishi wa mifumo ya ikolojia ya bahari na pwani, kuhamasisha matumizi ya Suluhisho Zinazotegemea Asili katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kupanua fursa za uchumi wa buluu kwa wanawake na vijana.

Nchini Tanzania, Mradi wa ReSea unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Mission Inclusion, IUCN Tanzania na Women Fund Tanzania Trust (WFTT), ukilenga kuhakikisha jamii za pwani zinanufaika na maendeleo ya kiuchumi yanayoenda sambamba na uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com