Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Wafanyabiashara zaidi ya 300 waliokuwa wakitegemea kipato chao kupitia Soko la Rehema Nchimbi jijini Dodoma, wamejikuta wakikaa kwa zaidi ya miezi saba bila kufanya biashara, hali iliyosababisha kudorora kwa maisha yao ya kiuchumi na kijamii, huku wakiiomba Serikali kuingilia kati mgogoro unaoendelea kati yao na uongozi wa Jiji la Dodoma.
Wafanyabiashara hao waliondolewa katika eneo lao la awali Oktoba mwaka jana kupisha matumizi mengine ya Bunge la Tanzania, lakini tangu wakati huo hawajapatiwa eneo mbadala linaloweza kutumika rasmi kwa shughuli zao za kila siku.
Wakizungumza Mei 2, 2026 katika eneo la Umonga waliloelekezwa kuhamia, wafanyabiashara hao walisema licha ya Serikali kupitia uongozi wa mkoa kuwatafutia eneo hilo kama suluhisho la muda na baadaye la kudumu, bado hawaruhusiwi kuanza biashara kutokana na kutokamilika kwa miundombinu muhimu pamoja na changamoto za kiutawala.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Prisca Chibwaye, alisema tangu walipoondolewa katika vibanda vyao, wamekuwa wakikabiliwa na maisha magumu kutokana na kukosa kipato, huku juhudi zao za kufuatilia haki yao ya kupata eneo la biashara zikikwama.
Alieleza kuwa waliondolewa bila fidia yoyote, na ingawa walipatiwa eneo la Umonga, bado halijawa tayari kutumika, jambo linalozidisha ugumu wa maisha yao ya kila siku.
Aidha, wafanyabiashara hao walikumbusha kuwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba mapema mwaka huu, alitoa maelekezo ya wazi ya kuliboresha eneo hilo kwa kumwaga kifusi, kulijenga miundombinu ya msingi na kulifanya kuwa eneo la kudumu la biashara. Hata hivyo, hadi sasa utekelezaji wa maagizo hayo haujakamilika.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wengi wamejikuta wakishindwa kulipa mikopo waliyochukua katika taasisi za kifedha, huku wengine wakilazimika kuuza mali zao binafsi ili kumudu mahitaji ya familia zao, ikiwemo ada za watoto na chakula.
Kwa upande wake, Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa soko hilo, Abdullah Gogo, alisema kufungwa kwa soko hilo Oktoba 29 mwaka jana kumeathiri moja kwa moja maisha ya wafanyabiashara hao, na kusisitiza kuwa changamoto kubwa si uamuzi wa Serikali kuhamisha soko, bali ni kuchelewa kwa utekelezaji wa maandalizi ya eneo mbadala.
Aliongeza kuwa pamoja na maagizo ya kumwaga kifusi kwa ajili ya kuboresha eneo hilo, kiasi kilichofikishwa ni kidogo na hakitoshi kukidhi mahitaji ya eneo lote, huku huduma muhimu kama maji, umeme na vyoo zikiwa bado hazijafikishwa.
Hata hivyo, uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma umeeleza kuwa ucheleweshaji wa matumizi ya eneo hilo unatokana na baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kusaini mikataba ya matumizi ya eneo hilo.
Kwa mujibu wa uongozi huo, mikataba hiyo ni muhimu ili kuruhusu matumizi halali ya eneo la Serikali, na hauwezi kupuuzwa licha ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao.
Katika mazingira hayo, wafanyabiashara hao wameendelea kusisitiza ombi kwa Serikali kuingilia kati kwa haraka ili kuweka mwafaka utakaowawezesha kurejea katika shughuli zao za kiuchumi, wakieleza kuwa kila siku inayopita inaongeza mzigo wa madeni na ugumu wa maisha kwao.



Social Plugin