
Na.Mwandishi wetu - Arusha
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), leo Mei 8, 2026 imefanya ziara katika Chuo cha Habari Maalumu Arusha kwa lengo la kutembelea idara mbalimbali za chuo hicho pamoja na kufanya muhadhara kuhusu historia ya vyombo vya habari na utendaji wake hapa nchini.
Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Bwana Edwin Soko, ambapo pia kulifanyika mazungumzo kati yake na Mkuu wa Idara ya Media chuoni hapo, Bwana David Mnkeni, kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya MISA Tanzania na chuo hicho kinachofundisha kozi mbalimbali za uandishi wa habari.
Majadiliano hayo yalijikita katika kuweka mikakati ya pamoja ya kuwaendeleza wanachama wa MISA na waandishi kwa ujumla kitaaluma pamoja na kushirikiana katika shughuli mbalimbali zinazolenga kulinda uhuru wa habari, uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Bwana Edwin Soko, aliipongeza menejimenti ya chuo hicho, walimu pamoja na wanafunzi kwa juhudi zao za kutoa na kupata elimu bora ya uandishi wa habari.
Soko aliwataka wanafunzi hao kuzingatia maadili ya uandishi wa habari wakati wote wa masomo yao na hata watakapohitimu na kuanza kufanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari.
“Ni muhimu kwa wanahabari wa baadaye kutambua kuwa taaluma ya habari inahitaji uwajibikaji, weledi na kuzingatia maadili ya kazi wakati wote,” alisema Soko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Media, Bwana David Mnkeni, aliishukuru MISA Tanzania kwa kufanya ziara chuoni hapo na kuonyesha utayari wa kushirikiana kwa karibu katika kukuza taaluma ya habari nchini.
Mnkeni alisema ushirikiano huo utasaidia kuwajengea uwezo wanafunzi na wanahabari kwa ujumla kupitia mafunzo, mijadala na shughuli mbalimbali za kitaaluma.




Social Plugin