Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZILITUMIKA PICHA NYINGI ZA AI KUONESHA MAUAJI OKTOBA 29 - JAJI CHANDE



Na mwandishi wetu, Dar es salaam

Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, 2025 Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema katika ushahidi wa kidijitali uliofanywa na Tume hiyo umethibitisha kuwa baadhi ya picha mnato na picha mjongeo zilizokuwa zikizunguka zaidi katika mitandao ya kijamii wakati wa matukio ya Uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 hazikuwa halisi, zikiwa zimechezewa na akiliunde (AI) kuaminisha watu kuwa ni picha halisi za maafa na vifo vilivyotokea wakati huo.

Jaji Chande amebainisha hayo leo Alhamisi Aprili 23, 2026 Ikulu Jijini Dar Es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi matokeo ya uchunguzi wa Tume hiyo kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitolea mfano wa picha hizo kuwa ni ile iliyosambaa ikionesha mifuko yenye maiti ambayo ilizikwa kwa halaiki.

"Tume tuliweza kutofautisha picha halisi na zisizo halisi kwa kutumia utaalamu, kwa mfano mojawapo ni picha ambayo imetumika mara nyingi kuonesha maiti zikiwa kwenye mifuko ya buluu zikizikwa kwenye makaburi ya halaiki. Picha hiyo kwa mujibu wa uchunguzi imetumika sehemu nyingi duniani." Amesema Jaji Chande.

Kulingana na Mwenyekiti huyo, matumizi ya ushahidi na taarifa mseto kutoka kwenye vyanzo anuai vilitumika zaidi na tume hiyo ili kulenga na kuthibiti viwango vya uthibitisho vinavyotambuliwa na Tume za uchunguzi za Kimataifa, wakizingatia pia kuwa na ushahidi wenye kujitosheleza.

Kulingana na Jaji Chande katika ushahidi wa kidijitali walifanikiwa kukusanya picha mnato 450 na picha mjongeo 880 kwa njia mbalimbali ikiwemo zile ambazo zilisambaa mtandaoni kwa zaidi ya mara moja, zilizowasilishwa na mashuhuda wa matukio, watoa taarifa wa Vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na picha kutoka kwenye vyanzo vya wazi ikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com