Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI WA DINI WATUUNGANISHE NA KUHIMIZA KUSAMEHEANA- SIMBAKALIA



Na mwandishi wetu, Dar

Kanali Mstaafu Joseph Leon Simbakalia amewaomba na kuwahimiza Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali nchini kutekeleza wajibu wao kikamilifu katika kuwaunganisha Watanzania pamoja na kuhimiza jamii kusameheana kama msingi muhimu wa kuendeleza Umoja wa Kitaifa, ushirikiano na mshikamano nchini Tanzania.

"Kubwa kabisa Viongozi wa kiroho kwa madhehebu yote watusaidie, la kwanza ni kutuongoza katika kujitathimini na kujisahihisha, pili ni kutujengea msingi wa kusameheana na hili ndilo Viongozi wa dini wanaotakiwa kuwajibika zaidi kwa kutuunganisha. Ni muhimu walau wakatenga siku moja tu katika kufanya maombi ya pamoja na kutuunganisha katika umoja huu tulionao kama Taifa." Amekaririwa Bw. Simbakalia.

Kanali huyo mstaafu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 02, 2026 wakati wa mahojiano yake kwenye kipindi kinachorushwa na runinga ya Channel Ten ya Jijini Dar Es Salaam, akisisitiza kuwa umoja, mshikamano na amani iliyopo nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 60 sasa imejengwa na kudumishwa tangu enzi za waasisi wa Taifa na ni jukumu la kila Mtanzania kuiendeleza na kuidumisha kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na kijacho.

Simbakalia ameyazungumza hayo wakati huu ambao Taifa chini ya serikali ya awamu ya sita linaelekea katika mchakato wa maridhiano ya Kitaifa, Viongozi wa dini wakitajwa kama daraja muhimu la kuponya majeraha ya kijamii, kisiasa, na kihisia kutokana na nyumba za ibada kukusanya watu wa makundi yote bila kujali tofauti zao za kisiasa.

Wakati huu wa kuhitimisha mfungo wa Kwaresma na kuanza msimu wa sikukuu za Pasaka, Viongozi wa dini pia wanahimizwa kutumia fursa hiyo kutoa wito wa msamaha na upendo, jambo ambalo ni chachu ya ushirikiano na umoja wa Kitaifa kama msingi wa ustawi wa jamii na maendeleo ya Nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com