Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ASHIRIKI KONGAMANO LA KITAIFA LA MAMA NA BABA LISHE JNICC



Na mwandishi Maalum, Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,ameshiriki kongamano la kitaifa la Babalishe na Mamalishe na kugua mabanda ya maonesho ya mapishi ya mama na baba lishe mara baada ya kuwasili katika Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), jijini Dar es Salaam, leo Aprili 21, 2026.

Rais Samia pia amepata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali yaliyoandaliwa na wajasiriamali hao, ambapo alijionea aina tofauti za vyakula vya asili na vya kisasa vinavyotayarishwa na mama lishe na baba lishe kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza kwa ufupi na washiriki wa maonesho hayo, Rais Samia amewapongeza kwa ubunifu wao katika mapishi na mchango wao mkubwa katika kukuza ajira pamoja na uchumi wa taifa. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha viwango vya usafi, ubora wa huduma na ubunifu ili kuvutia wateja zaidi na kuongeza thamani ya biashara zao.

Maonesho hayo ni sehemu ya kongamano linalowakutanisha mama lishe na baba lishe nchini, likiwa na lengo la kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za biashara na kuimarisha sekta ya chakula ambayo imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa wananchi wa kipato cha chini na cha kati.

Ujio wa Rais Samia katika tukio hilo umeongeza hamasa kwa washiriki, wengi wao wakieleza kufurahishwa na kitendo hicho cha kutambua na kuthamini juhudi zao katika kujipatia kipato na kuchangia maendeleo ya taifa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com