
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwezekaji, Dk. Tausi Kida, alibainisha kuwa uoanishaji wa mipango hiyo na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) ni hatua muhimu itakayohakikisha rasilimali zinazoelekezwa nchini zinaleta matokeo yanayopimika kwa wananchi, hususan kundi kubwa la vijana linalosubiri fursa za kiuchumi.
Katika mazungumzo na Kundi la Washirika wa Maendeleo (DPG) jijini Dar es Salaam, Dk. Kida alieleza kuwa kuanzishwa kwa Tume ya Taifa ya Mipango ni mageuzi ya kimkakati yenye lengo la kuimarisha uratibu na uwazi katika utekelezaji wa miradi. Alisisitiza kuwa ushirikishwaji wa mapema wa wadau hao ni nguzo ya kuhakikisha kuwa uwekezaji unaofanyika unachochea sekta za kipaumbele kama kilimo, viwanda, na nishati, ambazo ndizo injini kuu za kuzalisha ajira na kuimarisha mnyororo wa thamani kwa vijana nchini kote.
Naye Balozi Dk. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alibainisha kuwa serikali inathamini ushirikiano wa muda mrefu, lakini sasa ni wakati wa kuhakikisha miradi yote inalenga moja kwa moja matokeo chanya kwa maisha ya Watanzania.
Alisema kuwa mshikamano kati ya serikali na wafadhili unapaswa kuonekana kupitia programu zinazoongeza tija katika nguvukazi ya taifa, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukuza diplomasia ya kiuchumi inayozingatia maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wao, washirika wa maendeleo wakiongozwa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Susan Namondo, waliipongeza Tanzania kwa kuandaa Dira ya 2050 wakisema inatoa mwelekeo thabiti wa kisera unaovutia wawekezaji.
Aidha, Naibu Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Ireland, Suzanne Keatinge, alikumbusha kuwa siri ya mageuzi ya kiuchumi ipo katika kuwekeza kwenye elimu na ujuzi (rasilimaliwatu), akisisitiza kuwa nguvukazi yenye maarifa bora ndiyo inayovutia uwekezaji wa kigeni na kuunda ajira zenye staha kwa vijana, jambo ambalo ni msingi wa amani na utulivu wa taifa.
Social Plugin