Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM NA CHANGAMOTO YA VYAMA VINGI



 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliasisiwa mwaka 1977 kutokana na muungano wa vyama vya ASP na TANU. Msingi mkuu wa CCM ni falsafa ya ujamaa na kujitegemea, kama ilivyowekwa mkazo katika Azimio la Arusha. Aidha, chama hiki kinasimamia misingi ya utu, undugu na usawa katika jamii.

Dhamira na Malengo ya CCM

Kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa, lengo kuu la CCM ni kushika dola na kuunda serikali. Kwa muda mrefu, CCM imefanikiwa kutimiza lengo hili kutokana na kuendelea kuaminiwa na Watanzania. Imani hiyo inatokana na uimara wake katika kusimamia misingi, sera na utekelezaji wa ilani zake ambazo zimekuwa na manufaa kwa wananchi.

Mfumo wa Vyama Vingi Tanzania

Historia inaonesha kuwa mwaka 1992, iliundwa tume iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mfumo wa chama kimoja au vyama vingi. Matokeo yalionesha kuwa asilimia 79 ya wananchi walipendelea kuendelea na mfumo wa chama kimoja, huku asilimia 21 wakipendelea mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, sheria ya vyama vya siasa ilitungwa mwaka 1992, na mwaka 1995 Tanzania ilifanya uchaguzi wake wa kwanza wa vyama vingi. Tangu wakati huo, mfumo huo umeendelea hadi sasa.

Faida za Mfumo wa Vyama Vingi

  1. Kuongeza wigo wa demokrasia katika siasa.

  2. Kuchochea ushindani wa maendeleo.

  3. Kutoa fursa ya kukosoa na kuibua mbadala wa sera na mikakati ya maendeleo.

JINSI CCM INAVYOKABILIANA NA CHANGAMOTO YA VYAMA VINGI

1. Falsafa ya Kujitegemea
Kupitia Azimio la Arusha la mwaka 1967, CCM iliweka msingi wa kujitegemea kama taifa. Kwa sasa, sehemu kubwa ya bajeti ya serikali (zaidi ya asilimia 70) inatokana na mapato ya ndani yanayokusanywa na TRA pamoja na halmashauri. Hali hii inaongeza imani kwa wananchi juu ya uwezo wa CCM.

2. Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na Kijamii
Kupitia ilani zake, CCM imeelekeza serikali kuwezesha wananchi kiuchumi. Mfano ni utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum kupitia halmashauri. Hatua hii imeongeza ustawi wa wananchi na kuimarisha imani yao kwa chama.

3. Amani na Utulivu wa Nchi
Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani tangu kupata uhuru. Hii ni matokeo ya uongozi thabiti wa CCM katika kulinda tunu ya amani, jambo linalowezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii bila hofu.

4. Miundombinu ya Usafiri na Huduma za Kijamii
Nchi imeunganishwa kwa mtandao wa barabara za lami na kuimarisha usafirishaji na biashara. Hii ni ishara ya juhudi za CCM katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

5. Huduma za Afya na Elimu
Sera za CCM zimewezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kama elimu bila malipo na bima ya afya kwa wote. Pia kuna huduma za matibabu bure kwa wazee pamoja na mama na mtoto, hali inayoboreshwa ustawi wa jamii.

6. Mtandao Mpana wa Uongozi
CCM ina mfumo imara wa uongozi kuanzia ngazi ya shina hadi taifa. Mtandao huu unaifanya kuwa karibu zaidi na wananchi kuliko vyama vingine.

Hitimisho

Kwa ujumla, CCM inaendelea kuimarika kisiasa kutokana na utekelezaji wa sera zake, kuheshimu utawala bora, na kulinda uhuru wa maoni. Aidha, juhudi zake katika kupambana na maadui watatu wa maendeleo—ujinga, maradhi na umaskini—zinaonekana kupitia ujenzi wa shule, hospitali na utoaji wa mikopo kwa wananchi.

Hatua hizi zimechangia kukuza uchumi, kuboresha maisha ya wananchi na kuifanya CCM kuendelea kuaminiwa na Watanzania.

MAKALA HII IMEANDIKWA NA:
JOHN FRANCIS HAULE
MKUU WA SOKO LA SAMUNGE
JIJI LA ARUSHA
Simu: 0756717987


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com