Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKAKATI MPYA WA SERIKALI WAFUFUA MATUMAINI SEKTA YA MAKAA YA MAWE



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Serikali imeanzisha mkakati mpya wa kuifufua na kuipa nguvu sekta ya makaa ya mawe nchini, hatua inayolenga kuongeza mapato ya taifa na kuhakikisha rasilimali hiyo inawanufaisha wananchi kwa kiwango kikubwa zaidi.

Mkazo huo mpya unakuja sambamba na jitihada za kuboresha uratibu, kuondoa vikwazo na kuongeza ufanisi katika uzalishaji na biashara ya makaa ya mawe.

Akizungumza Machi 30, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Serikali inataka kuona mabadiliko ya haraka katika sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na wadau kuungana na kuanzisha chama chao kitakachorahisisha mawasiliano na Serikali.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha rasilimali za nchi zinachangia kikamilifu maendeleo ya wananchi.

Mavunde ameeleza kuwa changamoto zinazowakabili wadau wa sekta ya makaa ya mawe zinaweza kutatuliwa kwa urahisi endapo watakuwa na umoja imara utakaowapa nguvu ya pamoja katika majadiliano na Serikali.

Ameweka wazi matarajio yake ya kuona hatua ya kuanzishwa kwa chama hicho ikikamilika ndani ya wiki moja, akisisitiza umuhimu wa wadau kuwa na sauti moja.

Aidha, Waziri huyo amewataka wadau kuwasilisha mapendekezo yatakayolenga kuongeza uzalishaji na tija, huku wakihimizwa kuwa tayari kuyasimamia kwa vitendo.

Amesema Serikali iko tayari kushirikiana nao, ikiwa ni pamoja na kusaini makubaliano ya utekelezaji yatakayosaidia kufikia malengo ya pamoja.

Katika kuboresha mazingira ya biashara, Mavunde amegusia masuala mtambuka yanayohusisha Fedha na sekta ya uchukuzi, akieleza kuwa ushirikiano wa karibu ni muhimu ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa sekta hiyo.

Pia ameagiza Tume ya Madini kushughulikia kwa haraka malalamiko ya mrabaha ili kutoa ufafanuzi na kuondoa sintofahamu miongoni mwa wadau.

Kwa upande wa soko, Serikali imesisitiza kuwa haitakuwa tena ikiweka bei elekezi ya makaa ya mawe bila kushirikisha wadau, ikilenga kulinda ushindani na ufanisi wa biashara.

Sambamba na hilo, imetangaza uteuzi wa mratibu maalumu wa kushughulikia masuala ya sekta hiyo, hatua inayotarajiwa kuharakisha utatuzi wa changamoto na kuifanya sekta ya makaa ya mawe kuwa mhimili imara wa uchumi wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com